MKE MBARONI KWA TUHUMA ZA KUMCHINJA MUMEWE

0

 Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza linawashikilia watu watano akiwemo Mkazi wa Kijiji cha Kiliwi wilayani Kwimba, Hoka Mazuri (48) na wanaye wawili kwa tuhuma kumuua mumewe, Mange Washa (49).

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amewataja watoto wa mwanamke huyo wanaoshikiliwa kwa mauaji hayo kuwa ni, Masunga Mange na Paskali Mange.

Mutafungwa amedai, ili kufanikisha lengo lao bila kushtukiwa wanafamilia hao walimlipa mkazi wa Bugembe wilayani humo, Shija Masalu (28) na Makoye Lusana (53) Sh800, 000 ili wamuue baba wa familia hiyo ambaye taarifa zinadai alikuwa kikwazo wanapohitaji kutumia mali za familia hiyo.


Amesema Desemba Mosi mwaka huu Saa 1:00 usiku baada ya kulipwa fedha na familia hiyo, Masalu na Lusana walimvamia Mange Washa akiwa amelala wakamkata kichwa na kukitenganisha na kiwiliwili kisha kutokomea kusikojulikana.

"Mauaji ya Mange yalipangwa na mke wake akishirikiana na watoto wake wawili kutokana na ugomvi wa mali uliyodumu kwa muda mrefu, kwani mmoja wa wana familia hiyo, Masunga Mange alifukuzwa na baba yake (Marehemu) kwa kuhusika na wizi wa mifugo ya familia yake na ya wakazi wengine wa kijiji hicho.

"Baada ya mauaji hayo Hoka Mazuri na wanaye wawili waliwahadaa watoto wengine ambao walikuwa wamelala nyumba nyingine jirani kwamba, baba yao amekatwa mapanga na mtu asiyejulikana, wakati wanaujua ukweli kuwa wao ndiyo waliopanga na kuratibu mauaji hayo," ameongeza.

Amesema watuhumiwa hao wanaendelea kushikiliwa chini ya jeshi hilo kwa mahojiano zaidi na upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.

Katika hatua nyingine, Kamanda Mutafungwa amesema jeshi hilo kupitia doria zake linawashikilia watu 104 kwa makosa mbalimbali ikiwemo kukutwa na kilo 29 za Bangi, na miche 40 ya bangi, mirungi kilo 62.6, lita 4,270 za pombe aina ya Gongo, mitambo 14 ya kutengenezea pombe hiyo na gramu 2.3 za dawa za kulevya aina ya Heroine.


Pia, amesema watuhumiwa wengine 18 wanashikiliwa kwa tuhuma za makosa ya uvunjaji wa nyumba na maduka kisha kuiba mali zikiwemo televisheni, simu na pikipiki.

"Pia tumekamata vifaa mbalimbali vilivyoibwa katika mradi wa ujenzi wa daraja la JPM Kigongo-Busisi na nyavu haramu za kuvulia samaki ndani ya Ziwa Victoria," amesema Mutafungwa.


Katika tukio lingine, Kamanda Mutafungwa amesema jeshi hilo linamshikilia mkazi wa Mtaa wa Jiwe Kuu kata ya Kitangiri wilayani Ilemela mkoani hapa, Merry Seni (21) kwa tuhuma za kutoa ujauzito wenye umri wa miezi saba na kutupa kichanga hicho.

Chanzo;Mwananchi

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 


 

 




#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top