SIMANZI ZATAWALA MSIBA WA BW HARUSI ALIYEJINYONGA

0

Vilio na simanzi vimetawala kitongoji cha Saghana, Wilaya ya Moshi Mkoa wa Kilimanjaro, wakati wa kuagwa kwa mwili wa Dk Joseph Patrick Ngonyani anayedaiwa kujinyonga siku aliyopaswa kupeleka mahari kwa wakwe zake.

Aliyekuwa mchumba wa Ngonyani, Naomi Sila alishindwa kujizuia wakati wa kuaga mwili wa mpenzi wake, hali iliyosababisha kubebwa na kurudishwa kwenye gari.

Naomi akiwa ameambatana na ndugu zake, aliwasili eneo la kuaga mwili baada ya watu wote kumaliza shughuli ya kuaga na hata aliposhushwa kwenye gari, alikuwa akilia huku akiita Jose (Joseph) amka, kelele ambazo ziliamsha vilio kwa ndugu, jamaa na waombolezaji waliokuwepo, katika ibada hiyo fupi.

Akiwa ameshikwa na ndugu zake, alipelekwa hadi lilipokuwa jeneza lenye mwili wa mchumba wake, ambapo baada ya kuona picha iliyokuwa juu ya jeneza alilia kwa sauti huku akisema Jose amka, kwa nini umeniacha, usiende Jose, huku akitaka jeneza lifunuliwe ili auone mwili, hali ambayo hata hivyo haikuwezekana kuuona.

Akizungumza mdogo wa marehemu, Sebastian Ngonyani alisema marehemu ni mtoto wa kwanza katika familia yao yenye watoto wanne na mipango ya harusi ya ndugu yao ilikuwa imekamilika kwa zaidi ya asilimia 90.

"Siyo kwamba alishindwa kutoa mahari, hapana, kwani mipango yote ilishakamilika kwa zaidi ya asilimia 90 na pande zote mbili kwa upande wa mwanamke na mwanaume zilikuwa vizuri," amesema


Amesema mara ya mwisho kuwasiliana na ndugu yake ilikuwa Ijumaa Novemba 25, 2022 ambapo alimwambia Jumamosi anakwenda kumalizia shughuli zake kwa wakwe na ndipo iendelee mipango ya harusi.

"Niliwasiliana na kaka ijumaa, na aliniambia Jumamosi anaenda kumaliza shughuli kule kwa wakwe zake, na kilichobaki tuangalie sherehe yetu inaendaje ili kila kitu kiende vizuri.”


“Nilimtakia kila la heri na kumuuliza kama kuna shida akaniambia, dogo nilipofikia kila kitu kipo vizuri na kwangu ilikuwa heri kusikia hivyo, maana yule ni ndugu yangu na kila kitu huwa tunasaidiana," amesema

Dk Joseph Patrick Ngonyani (33) anadaiwa kujinyonga kwa kutumia shuka, nyumbani kwake alikokuwa akiishi, Novemba 26, 2022, siku ambayo alipaswa kupeleka mahari kwa wakwe zake kijiji cha Lotima, nchini Kenya.

Dk Ngonyani ambaye alikuwa akifanya kazi katika zahanati ya Saghana iliyopo nje kidogo ya mji wa Himo kata ya Makuyuni, alijinyonga ikiwa umebaki Mwezi mmoja kufika siku ya ndoa yake.


Imedaiwa sherehe ya kumuaga  bibi harusi mtarajiwa, huko kwao kijiji cha Lotima, ilikuwa imepangwa kufanyika Disemba 18 na harusi ilitarajiwa kufanyika Disemba 28, 2022, nyumbani kwa bwana Harusi huko Songea, Mkoa wa Ruvuma.

Chanzo cha Dk Ngonyani kujinyonga bado hakijajulikana. Mwili umesafirishwa kupelekwa Songea kwa ajili ya Maziko yanayotarajiwa kufanyika  Alhamisi Disemba 1, 2022.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top