Wananchi wametakiwa kutokuwa na muhali katika kuripoti vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi ili kuliepusha Taifa dhidi ya vitendo hivyo.
Mapema akitoa elimu kwa wananchi wa Shehia ya Kinyikani, kaimu Kamanda wa mamlaka ya kuzuia rushwa na uhujumu uchumi Zanzibar 'ZAECA' Mkoa wa Kaskazini Pemba Nassor Hassan Nassir, amesema miongoni mwa changamoto zinazorudisha nyuma mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi ni pamoja na muhali, hivyo amewataka wananchi kuwachana na tabia ya hiyo.
Aidha, kaimu Kamanda huyo ameeleza kuwa kutoa na kupokea rushwa ni Kosa kisheria na yeyote atakayekutwa na makosa hayo hatua Kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Nao baadhi ya wananchi waliyohudhuria katika mkutano huo, wamesema bado wanakabiliwa na changamoto ya kuombwa rushwa pindi watoto wao wanapo omba nafasi za ajira Serikalini, jambo ambalo linarudisha nyuma mapengo ya watoto kuweza kupata ajira.
"Miongoni mwa changamoto za rushwa zinazotukabili ni pamoja na kuombwa rushwa katika kuomba ajira, anakuja mtu anakuambia nipe kiasi fulani cha pesa ili nikusaidie Mtoto wako apate ajira na ukiangalia ajira unaitaka basi unajikuta tu unatoa pesa zinaliwa na ajira hupati, kwahivyo suala hili linarudisha nyuma sana kwakweli" Ali Amour Ali, mwananchi
Aidha, wananchi hao wameahidi kutoa ushirikiano kwa ZAECA katika kutokomeza vitendo vya rushwa vinavyorudisha nyuma maendeleo ya taifa na kuwanyima haki wananchi.
Kwa upande wake Sheha wa Shehia hiyo Mussa Rashid Said, ameishukuru taasisi ya ZAECA kwa kufika katika Shehia hiyo kutoa elimu kwa wananchi juu ya mapambano dhidi ya rushwa na uhujumu uchumi.
Siku ya rushwa duniani huadhimishwa December 9 kila mwaka, ambapo kwa Zanzibar itaadhumishwa katika Kijiji Cha Nungwi ikiwa na kauli mbiu ya "LAZIMA TUUNGANE KUTOKOMEZA VITENDO VYA RUSHWA DUNIANI"