MKURUGENZI Mtendaji wa Chama Cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar Dk. Mzuri Issa Ali, amesema, bado vyombo vya habari vitaendelea kuwa tegemeo kwa jamii, katika kuwabadilisha kutoka mtazamo finyu na kwenda wenye tija.
Dk. Mzuru aliyasema hayo leo Januari 23, 2023 wakati akifungua mafunzo pacha, kati ya waandishi wa habari wa Unguja na Pemba, kwa njia ya kielektroniki, kwenye mafunzo ya siku mbili, chini ya mradi wa Kuhamasisha hatua za kitaifa dhidi ya kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji, unaoendeshwa na tasisi zaTAMWA, KUKHAWA, TUJIPE, ZAFELA na ZAMWASO.
Alisema, vyombo vya habari ni jukwaa muhimu na limeshafanya mageuzi kadhaa, ikiwa ni pamoja na kusababisha kupatikana kwa sheria mbali mbali zikiwemo za kupinga udhalilishaji na adhabu zake.
Alieleza kuwa, ndio maana TAMWA katika kutekeleza kazi zote, lazima kuwashirikisha waandishi wa habari, ili kuhakikisha wanachotaka kukifanya, iwe rahisi kupata matokeo.
‘’Bado vyombo vya habari, vimekuwa eneo muhimu kwetu sisi wadau, kwa kule kufanya kazi zao kwa ufanisi, na kusababisha uwepo wa mabadiliko makubwa,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo Mtendaji wa TAMWA-Zanzibar Dk. Mzuri Issa Ali, aliwakumbusha waandishi hao, kuendelea kuibua changamoto za uongozi kwa wanawake, watu wenye ulemavu na fursa za kiuchumi kwa vijana.
Akizungumza kabla ya mafunzo hayo, Mratibu wa TAMWA-Pemba Fat-hya Mussa Said, alisema mradi huo, unalenga kuibua changamoto, hasa zinazowakwaza wanawake na watu wenye ulemavu, zinazopelekea wasifikie malengo yao.
‘’Kundi la vijana, wanawake na watu wenye ulemavu nayo yanahaki sawa kama yalivyo mengine, sasa iweje yakose kuaminiwa na jamii, ni wajibu wa vyombo vya habari kwenda kuona nini tatizo,’’alihoji.
Akiwasilisha mada ya ushiriki na ushirikishwa wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika siasa, uongozi, uchumi na fursa nyingine, mwanaharakati Sabah Mussa Said, alisema kama vyombo vya habari, vitatumia mbinu mbadala, makundi hayo yataishi kwa salama na Amani.
"Ili kufikia kiwango kizuri cha maendeleo katika Jamii zetu tunapaswa kuhakikisha kuwa Kila kundi linapaswa kushiriki na kushirikishwa katika Mambo mbali mbali iwe ni ya kijamii, kisiasa hata ya kiuchumi kwasababu hakuna ambaye haguswi na mambo hayo katika maisha yetu ya Kila siku, hivyo sisi kama wanaharakati na wanahabari tunapaswa kuunganisha nguvu za pamoja ili kuona jambo hili linazingatiwa" alisema
Alieleza kuwa, vyombo vya habari vimeshasababisha mabadiliko ya sheria na mitazamo mbali mbali, hivyo kama vitendelea kujengewa uwezo, makundi hayo yatapata haki za fursa zao.
Mwandishi wa Radio Jamii na Jamii TV Online Ali Massoud Kombo, alisema bado elimu ya kujitambua kwa vijana inahitajika, ili waaminiwe ndani ya jamii yao, pale wanapotaka kugombea nafasi mbali mbali.
"Bado Jamii haijawa na Imani Kwa vijana katika kushika nafasi mbali mbali za uongozi Kwa kile wanachoamini kuwa Vijana wengi hawana uelewa wa mambo napia hawajitambui, hivyo basi sisi kama wanahabari tuna jukumu kubwa la kuelimisha Jamii pamoja na Vijana wenyewe juu ya Kujitambua na kujithamini ili waweze kukubalika pindi wanapohitaji kugombea nafasi mbali mbali za uongozi" alisema
Mwandishi wa habari wa ZBC Pemba, Mchanga Haroub , alisema uwezeshwaji na ufuatiliaji kwa vyombo vya habari, ni jambo moja, linalohitajika kufanyika mara Kwa mara ili kuongeza uwelewa kwa wananchi.
Mwandishi wa Blog ya Pemba ya Leo Fatma Hamad, alisema moja ya changamoto ambayo inaendelea kujitokeza na makundi hayo kukosa haki zao, ni elimu ya kuondoa dhana potofu kwa jamii.
"Bado Jamii zetu zimegubikwa na Imani potofu Kwa wanawake na watu wenye ulemavu katika kushika nafasi za uongozi, Kwa kile wanacho amini kuwa mwanamke ni mama wa nyumbani na hatakiwi kujiingizia katika Mambo ya siasa na uongozi sambamba na kuwahisi watu wenye ulemavu kuwa ni watu wasioweza kufanya jambo lolote kutokana na Hali zao za ulemavu jambo ambalo sio sahihi"
Mradi huo wa miaka miwili, unafadhiliwa na taasisi ya Foundation For Civil Society, na unaendeshwa na Jumuiya ya wanasheria wanawek Zanzibar ZAFELA, KUKHAWA, Jumuiya Tumaini Jipya Pemba (TUJIPE), ZAMWASO na TAMWA Zanzibar.