Menyekiti wa taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation na mke wa Rais wa Zanzibar, mama Mariam Mwinyi, ameziomba taasisi na watu binafsi kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum ikiwemo watoto wenye ulemavu ili kuhakikisha wanapata haki zao muhimu ikiwemo haki ya malezi na elimu.
Mama Mariam Mwinyi, ameyasema hayo wakati akikabidhi vifaa mbali mbali kwa watu wenye ulemavu na mahitaji maalum katika Ukumbi wa Makonyo Wawi, amesema kuwawezesha watu wenye mahitaji maalum ni kuiwezesha jamii kwani watu hao wanamchango mkubwa katika kuleta maendeleo.
Aidha, ameipongeza taasisi ya My Hope Foundation kwa moyo wake wa dhati wa kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum visiwani Zanzibar ili kuhakikisha nao wanaishi katika mazingira mazuri.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mheshimiwa Matar Zahor Massoud, amesema jukumu la kuwapatia haki zao watu wenye ulemavu ni jukumu la kila mmoja, hivyo basi jamii inapaswa kuunganisha nguvu za pamoja katika utoaji wa haki hizo.
Nao walengwa wa msaada huo wameishukuru taasisi ya My Hope Foundation kwa kuwapatilia msaada huo na kuahidi kuvitumia vyema vifaa hivyo ili kuhakikisha lengo la utolewaji wa vifaa hivyo linafikiwa.
Jumla ya Viti Mwendo ( wheels Chairs) Saba vilitolewa watu wa Shehia ya Kisiwa Panza, Fimbo nyeupe (White Cane) sita kwa watu wa Michenzani na Chokocho na Magongo mawili Kwa wanashehia ya Chambani na Changaweni.
Msaada huo wa Viti mwendo, Magongo, Fimbo za kutembelea pamoja mikoba kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum umetolewa na taasisi ya My Hope Foundation kwa kushirikiana maafisa wa watu wenye ulemavu Mkoa wa Kusini Pemba.