AMRI YA MA DC YA KUWAWEKA WATU MAHABUSU SAA 48 ZIMEANZA KUWAINGIZA MATATANI

0

 Amri za wakuu wa wilaya za kuwaweka watu mahabusu kwa saa 48 zimeanza kuwaingiza matatani, baada ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Siha, Onesmo Buswelu, kuamriwa kulipa fidia ya Sh10 milioni na Serikali ikiamriwa kulipa Sh90 milioni.


Amri hiyo ilitolewa juzi na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, Lameck Mlacha akisema suala la Buswelu ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi, kumweka mahabusu kwa siku tano Marry Otaru (70) bila kumfungulia mashtaka yoyote ni haramu.

Otaru, ambaye ni mkurugenzi mwendeshaji wa Kampuni ya Otaru Manufacturing and Trading, aliwekwa mahabusu Desemba 24, 2019 na kuachiwa Desemba 25 mwaka huo.

Hata hivyo, alikamatwa tena Desemba 27 na kuachiwa Desemba 30 mwaka huo.

Hii ni hukumu ya pili kitanzi kwa wakuu hao baada ya Desemba 30, 2022, Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora kumpa ushindi Alexander Ntonge kumshtaki aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Komanya Kitwala.

Mkazi huyo alifungua kesi ya madai ya fidia ya Sh140 milioni dhidi ya Kitwala, akidai Januari 5, 2020, akiwa na askari wenye silaha za moto, alifika nyumbani kwa kwake na kuamuru akamatwe bila kosa lolote la jinai alilokuwa amefanya.

Alidai kuwa mkuu huyo alimdhalilisha mbele ya familia yake na kupelekwa mahabusu hadi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Safia Jongo alipoamuru aachiwe huru na alipofungua kesi hukumu ikaamuru alipwe Sh80 milioni.

Wimbi la wakuu wa mikoa na wilaya kuwaweka watu mahabusu na baadaye kuamuru kuachiwa bila kufunguliwa mashtaka lilikithiri zaidi wakati wa utawala wa Serikali ya awamu ya tano 2016-2020.

Akizungumzia hukumu hiyo, Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Profesa Edward Hoseah alisema hukumu hiyo inapeleka ujumbe kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria na kutaka wateule hao kurudi kwenye mstari.

Hukumu hiyo imekuwa gumzo katika mitandao ya kijamii, huku mawakili na watetezi wa haki za binadamu waliohojiwa na gazeti hili wakisema hukumu hiyo ni dalili kuwa, mambo yameanza kubadilika na nchi inarudi katika utawala wa sheria.

Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu Ruaha (Rucu), Dk Rwezaula Kaijage alisema Serikali inapaswa kumfilisi mkuu huyo wa wilaya kwa kuwa hakuelekezwa kufanya alichofanya, bali ni matumizi mabaya ya fedha za umma.

Mashtaka

Otaru alifungua kesi ya madai ya Sh350 milioni dhidi ya Buswelu kwa jina lake na pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Polisi (OCD), Wilaya ya Siha, Namsemba Mwakatobe.

Hata hivyo, mdaiwa huyo wa pili aliyekuwa OCD ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Trafiki (TRO) Mkoa Simiyu, Mahakama haikumtoza fidia kwa kuwa alikuwa akitekeleza amri.

Katika kesi hiyo, Otaru alimuunganisha pia, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kama mdaiwa wa tatu.

Kwa mujibu wa hati ya madai, Desemba 23, 2019 Otaru alikamatwa na OCD kwa amri ya mkuu huyo wa wilaya na kuachiwa kwa dhamana siku inayofuata na kukamatwa tena Desemba 27 na kuachiwa Desemba 30, 2019.Siku ya kwanza, mama huyo aliitwa ofisini kwa mkuu huyo wa wilaya na alipofika alikuta watu mbalimbali, akiwamo OCD na baadhi ya watendaji wa Chama Kikuu cha Wakulima wa Kahawa Kilimanjaro (KNCU).

Alitakiwa na Buswelu kujibu maswali yanayohusiana na ukodishaji wa shamba la chama hicho lakini alikataa kujibu kwa kuwa suala hilo lilikuwa mahakamani, ndipo mkuu huyo akamwagiza OCD amkamate na kumweka mahabusu.

Baadaye aliamuru aachiwe kwa dhamana na kumwagiza aende nyumbani akaandike hundi kwa KNCU, aliandika hundi hiyo ya Dola 4,000 za Marekani (Sh9.28 milioni) ingawa alikuwa hadaiwi kodi na chama hicho.

Watendaji wa chama hicho wakasema fedha hiyo ni kidogo lakini akasema hana fedha nyingine, ndipo Buswelu akaagiza tena awekwe mahabusu kwa siku nne na aliwekwa mahabusu yenye baridi, mbu na harufu kali ya kinyesi, hasa mkojo.

Ni kutokana na udhalilishaji na mateso hayo ndipo akafungua kesi kudai fidia.

Katika hukumu hiyo iliyotolewa Januari 25, 2023 na nakala yake kupakuliwa katika mtandao wa Mahakama juzi, Jaji Mlacha alisema watu wanaoshikilia ofisi za umma ni lazima waongozwe na Katiba ya nchi na sheria, katika utendaji wao.

“Siku zote ni lazima waheshimu viapo vyao vya ofisi na wajibu wa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria. Mahakama kama mhimili wa tatu wa Dola una wajibu wa kulinda Katiba na sheria za nchi,” alisema Jaji Mlacha katika hukumu hiyo.

Jaji Mlacha alisema katika hukumu hiyo amezingatia namna uhuru wa mdai (Otaru) na haki ya kwenda popote inayolindwa na Katiba ya Tanzania ilivyokiukwa na amezingatia pia umri wa mdai, hali ya mahabusu na mateso aliyoyapata.

TLS, LHRC, Jukata wafunguka

Rais wa TLS, Profesa Edward Hosea alisema Tanzania inaongozwa kwa misingi ya utawala bora unaoheshimu utawala wa sheria, hivyo ni vyema kila mwenye mamlaka asome sheria ili kujua mamlaka yake ili asiingie kwenye matatizo.

“Kazi za Ma-RC na Ma-DC ni kuleta maendeleo, hayo mambo ya kamatakamata waviachie vyombo vinavyohusika na uchunguzi na kukamata na sio kwa amri amri. Turudi kwenye mstari tujue hakuna aliye juu ya sheria.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC), Anna Henga alisema hukumu hiyo inatoa fundisho kwa watu wenye mamlaka na vyeo kutotumia vibaya mamlaka yao, akisema Buswelu alifanya uonevu.

“Kuna uonevu mkubwa sana unafanywa na baadhi ya kada hizi za uongozi (Ma-DC). Wanafanya kazi za mahakama, polisi ni wao, chombo cha uchunguzi ni wao. Wakuu wa wilaya wafahamu hawako juu ya sheria,” alisema Henga.

Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Wangwe alisema hukumu hiyo ni dalili inayoonyesha kuwa mambo yameanza kubadilika na itasaidia uwajibikaji wa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya.

“Baadhi ya wateule hawa wanatumia vibaya mamlaka zao za kuwaweka watu ndani kwa saa 48. Sheria inataka ukitoa hii amri uhakikishe ndani ya huo muda huyo mtu anafikishwa mahakamani kwa kosa hilo ulilomkamata nalo,” alisema Wangwe.

Mawakili wanena

Wakili Dk Rwezara Kaijage alisema hukumu hiyo ni muhimu kuwarudisha wateule kwenye msitari na watambue kuwa kwa mujibu wa mfumo wa utawala uliopo, hakuna mtu aliye juu ya sheria.

“Yeye kama Dola hakupaswa kumweka mtu zaidi ya saa 24 bila kumfikisha mahakamani kwa kosa uliloamuru akamatwe nalo. Walio na madaraka wajue uongozi ni dhamana, usiutumie kuumiza mtu kwa sababu una madaraka,” alisema Dk Rwezara ambaye pia ni Mhadhiri wa RUCU.

Wakili John Seka wa Dar es Salaam aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya kuisoma vizuri sheria hiyo ya kuwaweka watu saa 48 na kusema hukumu hiyo itafungua milango ya waliodhulumiwa kudai haki.

Wakili Patrick Paul wa mjini Moshi alisema maamuzi hayo yameeleza sababu za ukomo wa matumizi ya nguvu ya wakuu hao kutoa amri ya mtu kuwekwa kizuizini na kuonyesha wazi kuwa uvunjifu wa masharti hayo kisheria ni batili.

“Ni uamuzi utakaowasaidia wakuu wa wilaya, mkoa, polisi na wananchi kuelewa mipaka ya mamlaka ya watawala. Inaonyesha ni wakati gani kiongozi hawezi kujificha nyuma ya pazia la Serikali kwa matendo yake binafsi,” alisema wakili Paul.

Mbali na mawakili hao, lakini wakili David Shillatu alisema, “sheria ya kumweka mtu ndani kwa saa 48 ina vigezo vyake. Kimojawapo ni pale inapoonekana mlengwa anataka kuhatarisha amani ya nchi au eneo husika na RC au DC yupo pale. Amri inaweza kutolewa ili tu kulinda amani.”

Alisema hukumu hiyo itumike kuzifumbua macho taasisi zote zinazofanya kazi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba zitekeleze majukumu yao kwa mujibu wa sheria.

Wakili Peter Mshikilwa wa Dar es Salaam alisema sheria hiyo imeweka mipaka na ni pale tu anapohatarisha amani au uvunjifu mkubwa wa amani na atatakiwa kutoa sababu za kumshikilia huyo mtu, tofauti na hivyo ni uharamu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

JIUNGE NA IDAWA MEDIA SASA
Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Telegram na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka IDAWA TV Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube & Jiunge WhatsApp 

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top