Leonard Onyango Okoth wa umri wa miaka 14, Erick Otieno Okoth (12) na Joseph Onyango Omondi, mwenye umri wa miaka minane walikufa kifo cha uchungu baada ya baba yao wa kambo kuteketeza nyumba yao mtaa wa Korogocho nchini Kenya.
Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko ambaye alisaidia kusafirisha miili ya watoto hao hadi Kisumu kwa mazishi, alifichua kuwa mshukiwa alikuwa akimlenga mkewe wa zamani waliyetengana wakati wa shambulio la uchomaji moto lakini hata hivyo kusudio lake liliwakuta watoto hao badala ya mama yao.
Wavulana hao wasiokuwa na hatia ndiyo waligeuka wahanga wa shambulio hilo la kikatili ambapo walichomeka kiasi ya kutotambulika miili yao.
Wawili kati ya wavulana hao walikuwa wanawe wa kambo mwanamume huyo huku mwathiriwa mwingine akiwa mtoto wake asili.
"Lengo lake kuu lilikuwa kumuua mke wake wa zamani ambaye kwa neema ya Mungu hakuwa ndani ya nyumba wakati nyumba hiyo ikiteketezwa kwa moto na polisi bado wanamsaka mshukiwa ambaye bado yuko mafichoni," Sonko alifichua.
Katika video ya kuhuzunisha aliyoshiriki, familia inaonyeshwa ikiomboleza baada ya miili ya wavulana hao kuwasili nyumbani kwa mazishi.
Jamaa hao walionyeshwa wakitazama kwa uchungu majeneza ya watoto hao wachanga huku wakijiuliza ni kwa nini waliuawa kifo cha uchungu na cha ghafla kilichochochewa na mtu waliyemwita baba.