Tangazo la madalali wa kupiga mnada mali katika kaunti ya Kisumu limezua vichekesho vikubwa kwenye mitandao ya kijamii baada ya kampuni moja ya madalali kwa jina Nyaluoyo kutangaza kupiga mnada vitu mbalimbali kwa nyumba ya mpangaji mmoja aliyekwama kulipa kodi ya nyumba hiyo.
Madalali hao wa Nyaluoyo waliweka tangazo la kupiga mnada mali hiyo kwenye gazeti la Jumatatu Januari 30, 2023. Baadhi ya mali ambayo madalali hao walitangaza kupiga mnada ni pamoja na chupi za mwanamume na mwanamke waliokuwa wamepangisha katika nyumba hiyo.
Nyaluooyo walitoa wito kwa umma kujitokeza ili kuweka maombi yao ili kuuziwa chupi hizo, zikiwemo 4 za mwanamume, 4 za mwanamke, mabegi mawili ya watoto
Tangazo hilo lilikuwa linasema kuwa ni mzozo uliokuwa kati ya mmiliki wa nyumba na mpangaji wake kwa jina Zacharia Sichenje Masika.
Yeyote ambaye alitaka kuuziwa mali hiyo kutoka kwa mpangaji mkaidi alitaarifiwa kujitokeza katika ofisi za kampuni hiyo ya madalali mnamo Februari 7 saa tano asubuhi katika kaunti ya Kisumu.
Tangazo hilo lilionekana kwenye jarida moja la Jumatatu na wengi walilitupia vijembe kwa utani mwingi, wakisema kuwa hiyo ilikuwa kama njia moja ya kumdhalilisha mpangaji huyo na familia yake kwani hakuna mtu anayeweza kujitokeza kununua chupi zilizotumiwa wakati mpya sokoni huuzwa hadi kwa bei ya jioni ya shilingi mia tu.