Ubakaji ni ZIMWI linaloendelea kuwatafuna wanafunzi wengi katika visiwa vya Zanzibar katika karne hii ya 21.
Kwa mujibu wa ofisi ya mtakwimu mkuu wa Serikali ya Zanzibar,
matukio ya vitendo vya ubakaji ambayo yamekusanywa ikiwemo jeshi la Polisi,
mahakama na vituo vya mkono kwa mkono jumla ya matukio 1,363 sawa na asilimia
34.45 wanafunzi wamebakwa mwaka 2020.
Kwa upande wa Mkoa wa Kusini Pemba pekee ambapo Makala hii
ndipo inapoangazia vitendo vya ubakaji kwa watoto jumla ya matukio ya ubakaji
kwa watoto 272 yameripotiwa kutoka mwezi January hadi Disemba mwezi 2022, sawa
na asilimia 12.09.
TAKWIMU ZA WANAFUNZI WALIOBAKWA NA KUPEWA UJAUZITO KUANZIA JANUARY HADI JUNE, 2022.
Takwimu zilizotolewa na afisa mdhamin kutoka Wizara ya Elimu
na Mafunzo ya amali, zinasema takriban wanafunzi 11 wa Sekondari wamebakwa na 6
kati ya hao wamekupewa ujauzito na 5 wanaendelea na masomo.
Na jumla ya wanafunzi 7 wa Skuli ya msingi wamebakwa na mmoja kati ya hao ameshindwa kuendelea na masomo kutokana na kupata tatizo la ugonjwa wa akili.
Mkasa wa mwanafunzi wa darasa la saba mwenye umri wa miaka
15, mkaazi wa Jombwe Mwambe Wilaya ya Mkaoni Mkoa wa Kusini Pemba, ambaye March
27 mwaka 2022 familia yake ilimgundua mwanafunzi huyo kuwa na ujauzito wa miezi
saba na nusu na hatimae May 10,2022 alijufungua na kushindwa kuendelea na
masomo.
JE, WAZAZI NA WALEZI
WANAFAHAMU JUKUMU LAO KATIKA KUWAKINGA WATOTO WAO DHIDI YA VITENDO VYA UBAKAJI?
Ilikufahamu wazazi na walezi ni kwa namna gani wanafahamu
jukumu lao katika kuwalinda watoto wao dhidi ya vitendo vya ubakaji mwandishi
wa Makala hii alifanikiwa kuzungumza na baadi ya wazazi na walezi wa Mkoa wa
Kusini Pemba, ambapo wazazi watatu kati ya wanne ambao mwandishi wa Makala hii
alifanikiwa kuzungumza nao wamesema wanafahamu vyema jukumu katika kuwalinda
watoto wao dhidi ya vitendo vya ubakaji ingawa wamesema kukithiri kwa vitendo
hivyo inatokana na mabadiliko ya dunia ikiwemo matumizi ya simu za mkononi.
Ali Omar Juma miaka 67, ni baba wa watoto nane na mkaazi wa
Wawi Chake Chake, amesema akiwa kiongozi wa familia ana wajibu na jukumu la
kufuatilia mienendo ya watoto wake kwa kushirikiana na mke wake kuanzia kuamka
kwa watoto wao hadi wanalala lakini miongoni mwa changamoto wanazokumbana nazo
ni marafiki wabaya wa mitaani pamoja na Shuleni ambao kwao ni vigumu kuweza
kuwatambua.
“Mimi kama kiongozi wa
familia nafahamu vyema sana jukumu langu la kuhakikisha nawalea watoto wangu
katika maadili mema ili kuwalinda dhidi ya vitendo vya ubakwaji lakini unajua
kuna mambo mengi sana zinazosababisha kutokea kwa vitendo miongoni mwa hivyo
ikiwemo marafiki wa wabaya, matumizi mabaya ya simu pamoja na vishawishi
ukiachana na wale ambao wanabakwa kwa kutumiwa nguvu” alisema
Idrissa Bai Pandu miaka 58 mkaazi wa Chambani Wilaya ya Chake
Chake Pemba, ambaye ni baba wa mtoto ambaye amebakwa, amesema wameathiriwa sana
kitendo cha mtoto wake aliyekuwa kisoma kidato cha kwanza kubakwa na kukatishwa
kwa ndoto zake baada ya kukatisha kuendelea na masomo wakati akiwa kidato cha
tatu baada ya kupata tatizo la akili.
“Mwanangu alikuwa
anafahamu vizuri tu na alikuwa anapenda kusoma na alikuwa ana ndoto nyingi sana
ikiwemo kuwa mwanasheria lakini ndoto hizo zote zimepotea kutokana na kushindwa
kuendelea na masomo baada ya kubakwa kwa nguvu kwani kitendo alichofanyiwa
kilimfanya kila anapokutana na watu wengi kujisikia vibaya na kuwa kama mtu
aliyechanganyikiwa”
alisema
VIONGOZI WA DINI\OFIAI YA MUFTI.
Katika kupambana na vitendo vya ubakaji nchini viongozi wa
dini nao wanajukumu kubwa la kuhakikisha vitendo hivyo vitokomezwa.
Lakini je, wanafahamu dhima na wajibu wao katika jamii katika
kuielimisha jamii ili kukabiliana na vitendo vya ubakaji?
Akieleza dhima na wajibu wa viongozi wa dini katika kupambana
na vitendo vya ubakaji, Naibu katibu kutoka ofisi ya mufti mkuu kisiwani Pemba,
Sheikh Said Ahmad Mohammed, amesema wamekuwa na utaratibu wa kutoa mafunzo juu
ya vitendo vya ubakiji kwa walimu wa madrasa kila baada ya miezi mitatu ili
kuhakikisha walimu wa madrasa wanapata elimu hiyo kusudi waweze kuitoa kwa
wanafunzi.
Sambamba na hayo, aliongeza kuwa wamekuwa na program za kutoa
elimu ya kupambana na vitendo vya ubakaji kwa wananchi kupita maeneo wanayoishi
pamoja na vyombo vya habari ili kuweza kuwafikia wananchi wengi Zaidi katika
kupambana na vitendo vya ubakaji.
“Kiujumla Ofisi ya
mufti Kisiwani Pemba imeandaa program nyingi sana katika kupambana na vitendo
vya ubakaji, miongoni mwa program hizo ni kutoa mafunzo kwa walimu wa madrasa, kupita
mitaani pamoja na kutumia vyombo vya habari kusudi kuhakikisha wananchi wanapata
uelewa wa kutosha kupambana na vitendo vya ubakaji” alisema
WALIMU WA MADRSA.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Mufti Mkuu Kisiwani Pemba, jumla ya
walimu wa madrasa 7 wametuhumiwa kwa vitendo vya ubakaji wa wanafunzi wao mwaka
2022, ambapo walimu 3 kati ya hao walikutwa na hatia na kuhukumiwa kutumikia
vifungo mbali mbali ikiwemo mwalimu wa madrasa wa Ali Ussi Simai mkaazi wa
Mchwake Mwambe ambaye alimbaka mwanafunzi wake wa madrasa na kuhukumiwa miaka 15
na mahakama maalumu ya kupambana na makossa ya udhalilishaji Mkoa wa Kusini
Pemba.
MAHAKAMA
Kwa mujibu wa ofisi ya mwendesha mashtaka wa Serikali Mkoa wa
Kusini Pemba, jumla ya kesi 128 za ubakaji mwaka 2022 zilifikishwa Mahakama ya
Mkoa Chake Chake ambapo kati ya kesi hizo 97 zilitolewa hukumu na kesi 56
washtakiwa walikutwa na hatia na kuhukumiwa kutumikia vifungo pamoja na kulipa
fidia.
Kati ya kesi hizo 128 zilizowahusisha wanafunzi wa msingi na
sekondari, jumla ya wanafunzi 33 wameshindwa kuendelea na masomo kutokana na
kupewa ujauzito sambamba na kukutwa na matatizo kiakili na maradhi ya wasi
wasi.
Mwendesha mashtaka wa Serikali Ali Amour Make alisema “Kwa mujibu wa takwimu tulizonazo ukiangalia mwaka 2022 idadi ya matukio ya ubakaji kwa wanafunzi yamekuwa mengi Zaidi kuliko mwaka 2021, ambapo takwimu zetu zinaonesha takriban kesi 128 ziliripotiwa katika mahakama yetu ikilinganisha na mwaka jana ambapo kulikuwa na kesi 88, hivyo hii inadhihirisha kuwa bado suala la ukakaji ni donda ndugu katika visiwa vyetu vya Zanzibar licha ya Mheshimiwa Rais wa Zanzibar kuanzisha mahakama maalum ya kupambana na makosa udhalilishaji”
Wanaharakati na wadau wa kupambana na vitendo vya ubakaji
wanafanya kazi kubwa katika kuhakikisha vitendo vya ubakaji vinatokomezwa
ikiwemo kukutana na waandishi wa habari, kufanya makongamo na mijadala mbali
mbali katika kulitafutia moarobaini gonjwa hili ambalo linaonekana kadri siku
zinavyosonga likikatisha ndoto za watoto wakike Visiwani Zanzibar.
Mratibu wa Chama cha Waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA) Pemba Fat-hia Mussa Said alisema “Sisi kama wanaharakati wa kupambana na vitendo vya udhalilishaji ikiwemo ubakaji tumekuwa tukifanya program mbali mbali ikiwemo kukutana na wadau, waandishi wa habari, walimu wa madrasa, viongozi wa dini, vipeperushi, kampeni mbali mbali, makongamano na mijadala ili kuhakikisha wananchi wanapata uelewa katika kukabiliana na vitendo hivyo na kwa kiasi Fulani tunasema tumepiga hatua kwasababu licha ya kuona matukio ya ubakaji yameongezeka lakini hiyo imetokana na wanachi kutoa taarifa pindi yanapotokea matukio ya ubakaji sambamba na vyombo vya habari kuripoti matukio hayo”