Mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji yamekuwa yakikabiliwa na changamoto kadhaa, miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na sheria ambazo zinaonekana kuwa na mapungufu mbali mbali katika utekelezaji wake.
Sheria nambari 4 ya mwaka 2005 ya kulinda wari na watoto
waliozaliwa na mzazi mmoja pamoja na kutoa tafsiri halisi ya mwari, ni miongoni
mwa sheria yenye kasoro kadhaa ikiwemo tafsiri halisi ya mwari,
kuwaruhusu vijana kufanya mapenzi nje ya ndoa kwa sharti la mwanamke kutokupata
ujauzito, hukumu Kwa upande wa mwanamke kuwa ndogo na wengine kusema ni hukumu kandamizi dhidi ya wanawake pamoja na adhabu kuwa ndogo kwa upande wa mwanamme.
kwa mujibu wa tafsiri ya sheria hiyo mwari maana yake ni
mwanamke ambae hajaolewa na ambae mwenye umri wa miaka 18 mpaka 21 na ambae
hajazaa.
Hukumu ya kosa la kumpa ujauzito mwari Kifungu cha 3 (3) kimeeleza
kuwa “aliyempa mimba mwari, atumikie chuo cha mafunzo kwa muda usiozidi miaka 3
na usiopungua miaka 5.
Kifungu 3 (6) mwari aliyepewa mimba atatumikia jamii kwa
kipindi cha miezi 6 kuanzia miezi mitatu baada ya kujifungua.
WANANCHI WANASEMAJE KUHUSU SHERIA HII?
Idawaonline.com imezungumza na wananchi mbali mbali kuhusu
sheria hii, ambapo baadhi ya wananchi wamesema mapungufu katika sheria hiyo ni
kutofautiana kwa adhabu kati ya mwanamme na mwanamke jambo ambalo sio sahihi
kwa vile wote ni watu wazima na wamefanya tendo la ndoa kwa makubaliano.
Juma Said Khatib miaka 48 mkaazi wa Shehia ya Wara, amesema
kutofautiana na kwa adhabu kunapelekea kuongezeka kwa vitendo vya hivyo kwani
adhabu hizo haziwafanyi wanawake kupata mabadiliko ya kitabia.
“Binafsi sikubaliani na
Sheria hiyo ya adhabu kwasababu kama mwanamke ni mtu mzima kisheria hajalishi
kama amewahi kuolewa ama laa sheria inatakiwa kutoa adhabu sawa kwa upande wa
mwanamme na mwanamke endapo wamekubaliana” alisema
Kwa upande wa wanaharakati wa kupinga vitendo vya
udhalilishaji Kisiwani Pemba, wamesema adhabu ya kutumikia kifungo miaka 3 na
usiopungua miaka 5 ni ndogo hali inayopelekea kuongezeka kwa matukio ya
udhalilishaji.
“Kwakweli adhabu katika
Sheria hii bado ni ndogo sana maana ukiangalia miaka mitatu hadi mitano kwa kupoteza
heshima na thamani ya mtu ukizingatia katika karne hii miaka inakwenda speed
sana, kwahivyo sisi kama wanaharakati wa kupambana na vitendo vya udhalilishaji
tunapendekeza sheria hii ifanyiwe mabadiliko ili kuhakikisha watoto wakike na
wanawake wanatimiza ndoto” alishauri
Mkurugenzi wa jumuiya Tumaini Jipya Pemba(TUJIPE) Tatu
Abdalla Msellem, ameshauri kuondolewa kwa adhabu ya miezi sita kwa upande wa
wanawake kwani kuwepo kwa adhabu hiyo inazidi kuwakandamiza wanawake ambao
wanaopewa ujauzito ikizingatiwa kuwa wanawake wanaojifungua nje ya ndoa wanapitia
wakati mgumu wa matunzo yake pamoja na mtoto.
“Mimi nadhani kuwepo
kwa sheria ya adhabu ya miezi sita kwa wanawake wanaojifungua nje ya ndoa ni sheria
inayozidi kuwaongezea maumivu na fedheha wanawake kwani inawapa nafasi wanaume
kuendelea kuwadhalilisha wanawake” alisema
Mratibu wa Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania
(TAMWA) Kisiwani Pemba Fat-hiya Mussa Said, amesema upo wa Sheria za
udhalilishaji zenye mapungufu zinapelekea kukwamisha juhudi za mapambano dhidi
ya vitendo hivyo.
Aidha, mratibu huyo ameviomba vyombo vya habari kuongeza
nguvu katika kuandika habari na Makala mbali mbali zinazoshikiza kufanyiwa
marekebisho Sheria hizo.
“Vitendo vya udhalilishaji limekuwa ni janga kwa taifa kiasi kwamba kila siku tunaposikiliza vyombo vya habari tunasikia taarifa kuhusu vitendo hivyo, hivyo basi zile sheria zote ambazo zinaonekana kurudisha nyuma juhudi dhidi ya mapambano ya vitendo vya udhalilishaji zinapaswa kufanyiwa marekebisho haraka iwezekenavyo” Mratibu Tamwa Pemba.
WAANDISHI WA HABARI
Waandishi wa habari nao ni wadau wakubwa katika kuzifanyia
uchechemuzi sheria za udhalilishaji ambazo zinaonekana kuwa na mapungufu mbali
mbali katika utekelezaji wake.
Waandishi wa habari nao wamesema sheria namba 4 ya mwaka 2005
ya kulinda wari na watoto waliozaliwa na mzazi mmoja ni sheria inayokinzana na
misingi ya dini, mila na desturi za wazanzibari kwa kutokuwatia hatiani watu
wanaofanya mapenzi nje ya ndoa endapo kama mwanamke hakupata ujauzito, hivyo
wameomba kufanyiwa marekebisho kwa sheria hiyo na badala yake kutendo cha
kufanya mapenzi nje ya ndoa iwe ni kosa hata kama mwanamke hatopata ujauzito.
“Binafsi nikiwa kama
mtetezi wa jamii sikubaliani na sheria hii kwasababu asilimia 99 ya Wazanzibari
ni waumini wa dini ya Kiislamu pamoja na dini ya Kikristo mila na desturi
ambazo zote hazikubaliani na tabia ya kufanya mapenzi nje ya ndoa, kwahivyo naomba
sana sheria hii ibadilishwe badala ya kwamba kufanya mapenzi nje ya ndoa iwe ni
kosa kisheria kama ilivyo kwenye dini hata kama mwanamke hakupata ujauzito” Salum Ali Msellem, mwandishi wa radio
Istiqama Pemba
Suala la usawa wa adhabu ni miongoni mwa nukta ambazo
zimegusiwa katika sheria hiyo, ambapo mwandishi wa habari wa ZBC Pemba Hadija
Kombo Khamis, amependekeza wanawake kupewa adhabu sawa na ile wanayopewa
wanaume kwani kuwepo kwa utofauti wa adhabu kunachangia kwa kiasi kikubwa kukoma
kwa vitendo vya udhalilishaji.
“Mimi nadhani suala la
kutofautiana kwa adhabu ni suala linalohitaji marekebisho kwasababu haiwezekani
mwanamke mtu ambaye anafahamu kuwa kufanya mapenzi nje ya ndoa ni kosa kisha
baada ya kupata ujauzito mwanamme apewe adhabu kali na mwanamke apewe adhabu
nyepesi hii sio sahihi kabisa kwani juhudi za kutokomeza vitendo vya
udhalilishaji haitozaa matunda” HADIJA KOMBO ZBC
MAHAKAMA
Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka wa Serikali kutoka ofisi ya
Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar Ali Amour Makame, amesema sheria namabri 4 ya mwaka 2005 ni miongoni mwa Sheria zinazolalamikiwa kuwa na mapungufu
kutokana kukinzana na dini, mila na desturi za Wazanzibari katika kupambana na
vitendo vya udhalilishaji.
“Ni kweli kwamba Sheria hii ina mapungu kadhaa ikiwemo kutofautiana kwa adhabu baina ya mwanamme na mwanamke jambo ambalo wanasema sio sahihi lakini pia suala la kufanya mapenzi kutokuwa ni kosa na badala yake baada ya mwanamke kupata ujauzito pekee kuonekana ndio ni kosa” alisema
Ni matumaini ya mhariri wa Makala hii kuwa endapo Sheria hii itafanyiwa
marekebisho itaondosha malalamiko ya wananchi sambamba kuwarahishia kazi
wanaharakati wanaopambana dhidi ya vitendo vya udhalilishaji visiwani Zanzibar.