Mkazi wa Kitongoji cha Lugolofi, Kata ya Mapanda, Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, lkomeni Mbugi amenusurika kifo baada ya watu wasiojulika kumshambulia nyumbani kwake kwa kumkata na panga sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo kutenganishwa kiganja cha mkono wake.
Akizungumza Alhamisi Machi 2,2023, Mtendaji wa Kata ya Mapanda, Isaya Mweni amethibisha kutokea kwa tukio hilo huku akisema hatua mbalimbali za kuwabaini wahusika waliofanya tukio hilo zinazoendelea.
Mweni ameeleza kuwa tukio hilo limetokea Februari 28 mwaka huu Kitongoji cha Lugolofi inaelezwa kuwa Mbugi alishambuliwa kwa mapanga akiwa nyumbani kwake.
"Nilipata taarifa ya saa nne usiku kutoka kwa Mwenyekiti wa kitongoji kwamba Mkazi wa Kitongoji cha Lugolofi kuna mtu amejehuriwa na mapanga na watu wasiojulikana kwa kukatwa na mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake," amesema Mtendaji huyo.
Mweni amefafanua kuwa sababu za watu hao kufanya kitendo hicho bado hazijafahamika huku akitoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake wanatakiwa kuripoti katika vyombo husika ili hatua stahiki ziweze kuchumuliwa.
Kwa upande wake Mganga wa zamu wa Hospitali ya Mafinga Mji, Dk Lazaro Mtuya amethibisha kumpokea mgonjwa huyo saa 12:00 asubuhi akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili.
"Saa 12:00 asubuhi jana tulimpokea mgonjwa akitokea Kata ya Mapanda akieleza kwamba ameshambuliwa," amesema Mtuya.
Hata hivyo Dk Mtuya ametaja sehemu ambazo mgonjwa huyo alikuwa na majeraha kwamba ni kichwani, mkononi, miguuni pamoja na mkono wa kushoto kiganja chake kikiwa kimetenganishwa.
TAZAMA VIDEO HII KUHUSU WANAOTUMIA WHATSAPP