Marehemu ataka chanzo cha kifo chake aulizwe mama yake!

0

Mkazi wa Pasua Matindigani, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Godson Mbwambo (30) amefariki dunia kwa kujinyonga huku akiacha ujumbe unaodaiwa aliuandika ukutani kabla ya kuchukua uamuzi huo akieleza sababu za kifo chake aulizwe mama yake.Inadaiwa Alhamisi ya Februari 23, 2023 kijana huyo alijaribu kujiua kwa kujinyonga katika nyumba mbovu iliyopo jirani na kwao lakini aliokolewa na wenzake.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa hakupatikana kuzungumzia tukio hilo, kwa kuwa simu yake iliita bila kupokelewa.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Matindigani, Amosi Chibago amesema kijana huyo kajinyonga baada ya kujifungia katika chumba ambacho ukutani paliandikwa, “kifo changu muulizeni mama yangu."

Amesema kijana huyo anaishi nyumbani kwao na mama yake mzazi, wadogo zake pamoja na wapangaji, lakini alijinyonga katika chumba ambacho hakuwa akiishi mtu.

"Jumamosi nilipigiwa simu na balozi akinieleza kijana anayeitwa God amejinyonga, nilienda hadi eneo la tukio na nilipochungulia kupitia dirisha nilimuona tayari ameshafariki, lakini cha kusikitisha, ukutani alikuwa ameandika, ‘kifo changu muulizeni mama yangu," amesema.

"Chumba alichojinyongea hakiishi mtu kwani hakijamalizika vizuri, lakini niliambiwa siku ya Alhamisi kijana huyo alijaribu pia kujinyonga kwenye jumba bovu karibu na kwao na watu wakaenda kumuokoa," amesema.

Mwenyekiti huyo amesema,"Nimezungumza na mama yake anasema walishagombana siku za nyuma kidogo lakini hapa karibuni walikuwa wako shwari, lakini wenzake wanadai kwenye malalamiko yake kijana huyo alikuwa akimlalamikia mama yake kumnyanyasa na kwamba anachukua fedha anawapa watu wengine na yeye hampi kama vile hapo si kwao."

Aidha, mwenyekiti huyo ameshauri jamii, inapotokea mtu ametishia kujiua au kutamka maneno ya kutaka kujiua ni vizuri wakakaa nae karibu kujua kinachomsibu, ili kumuondolea msongo na dhamira aliyo nayo badala ya kumuacha hadi anachukua uamuzi kama huo wa kujiua.

Balozi wa eneo hilo, Albina Mushi amesema, kumewahi kutokea tatizo kati ya marehemu na dada yake na alipofuatilia ilionekana kuna tatizo katika mirathi.

"Hapo nyuma lilishatokea kijana huyu (marehemu ) na dada mtu kupigana na tatizo ilikuwa ni mambo ya mirathi ambapo marehemu alikuwa anauliza mbona wengine umeshawaingizia hela bado mimi hajaniwekea na baadae dada mtu alimpiga, lakini mama yake alinielezea hilo na nikaahidi ningemtafuta huyo kijana niongee nae ila ilikuwa bado sijaongea nae hadi tukio hili limetokea," amesimulia.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Pasua, Pastori Minja amesema tukio hilo limewasikitisha na kwamba bado chanzo cha kifo hicho hakijafamamika.

"Kifo hiki kimetusikitisha sana, maana kijana yule tulikuwa tukiishi naye hapa mtaani na alikuwa hana shida na mtu, sasa kilichomsibu hadi kuchukua maamuzi yale ya kujiua hatujui licha ya kwamba aliandika ukutani, kifo chake aulizwe mama yake,".

KAMA UNATUMIA WHATSAPP VIDEO HII INAKUHUSU
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 

 

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top