Mwalimu Mkuu mbaroni kwa madai kifo cha mwanafunzi

0

 Mwanafunzi aliyefariki dunia ni wa Glory Faustine (14) wa kidato cha kwanza huku  Emmanuel Liatu (13) akivunjika mguu, baada ya kudondokewa na jiwe wakati wakitekeleza adhabu ya Mwalimu Mkuu ya kuchimba changarawe. Adhabu hiyo  ilitolewa jana shuleni hapo.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Wilbroad Mutafungwa, alisema wanamshikilia mwalimu mkuu huyo pamoja na mwalimu wa zamu, ambaye jina lake hakulitaja.

Alisema wanamshikilia mwalimu wa zamu kwa kuwa ndiye mwenye jukumu la kujua ratiba zote za wiki ikiwa ni pamoja na adhabu zinazotolewa na usalama wa wanafunzi wanaozitekeleza.

Kamanda Mutafungwa alisema kutokana na kifo cha mwanafunzi huyo, shule hiyo imefungwa kwa muda ili kuzuia taharuki ambayo imejitokeza na kuwataka wananchi kuwa watulivu wakati taratibu za kisheria zikiendelea kufanyika dhidi ya wahusika waliosababisha jambo hilo.

Alisema tukio hilo lilitokea siku hiyo majira ya saa 3:00 asubuhi wakati wanafunzi wakichimba changarawe na ghafla waliangukiwa na jiwe lililosababisha kifo na kujeruhi mwanafunzi mmoja.

Kutokana na tukio hilo, wananchi wa maeneo hayo waliandamana ili kupata mwafaka  na kuitaka serikali kuondoa adhabu kali dhidi ya wanafunzi.

Mwanafunzi Jackline Jovin, ambaye ni miongoni mwa wanafunzi waliokuwa wakitekeleza adhabu hiyo, aliiambia Nipashe kwamba wakati wanaendelea na kazi hiyo waliona mawe madogo yakidondoka kwenye shimo walilokuwa wakichimba kwa ajili ya kupata changarawe.

“Tulitoka shimoni, mwenzetu alikataa kutoka akidai atatoka pindi atakapomaliza. Wakati  tunatoka ndipo jiwe likaporomoka na kumwangukia kichwani Glory na jiwe hilo lilimkandamiza mguu Emmanuel wakati akitoka,” alisimulia.

Getrude Michael, mzazi wa moja ya mtoto aliyekuwa akishiriki katika adhabu hiyo, alisema shule hiyo imekuwa ikitoa adhabu kali zinazopita uwezo wa wanafunzi na kuiomba serikali kuweka utaratibu mzuri wa utoaji adhabu kwa wanafunzi ili kuondoa matukio yanayosababisha madhara dhidi yao.

“Hii sio mara ya kwanza kwa shule hii kutoa adhabu kali. Zimekuwa  zikitolewa adhabu kubwa ikiwa ni pamoja na kubebeshwa matofali, kuchimba na kuhamisha vifusi na kuwaathiri kisaikolojia wanafunzi,” alisema.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kitangiri, Reuben John, alisema kutokana na jiografia ya mtaa huo wenye miamba mikubwa, hivi karibuni walifariki dunia watu baada ya kuangukiwa na mwamba wakati wakiendelea na shughuli za uchimbaji wa mawe. Alisema ajali za namna hiyo mpaka sasa katika mtaa huo zimeshatokea nne.

Muda mfupi baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji walifika na kuchukua mwili wa mwanafunzi huyo pamoja majeruhi na kuwapeleka katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa ya Sekou Toure.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 


 

 
#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top