Polisi kaika kaunti ya Homa Bay wanamshikilia mwanamume mmoja baada ya mke aliyerithi kutoka kwa marehemu kaka yake kufariki wakati walikuwa wanashiriki mapenzi.
Inaarifiwa kwamba wapenzi hao wawili walikuwa wameondoka kwenda katika sehemu ya starehe kujiburudisha na alfajiri waliporudi, hawakufika nyumbani.
Waliamua kupitia katika kichaka kilichoko karibu na boma lao ili kukata kiu cha mapenzi kidogo lakini katika tukio hilo, mwanamke yule alifariki.
Baada ya kufariki, mwanamume yule aliubeba mwili wake na kuuzika katika shimo shambani mwa jirani yao.
“Baada ya kunywa, walipanda pikipiki jioni lakini wakateremka katika kijiji cha Got Rateng A, mita chache kutoka nyumbani. Mshukiwa anaripotiwa kurithi Milca baada ya mumewe kufariki,” taarifa ilisema.
Kulingana na chifu wa lokesheni ya Lambwe Mashariki Bernard Ouma, mshukiwa alisema hakujua kuwa marehemu angefariki wakati wa kujamiiana. Ouma alisema walifanya mapenzi kwenye kichaka karibu na nyumba yao.
"Tulimkamata mshukiwa baada ya kukiri kwamba wamekuwa wakifanya mapenzi lakini kisa hicho kilitokea katika uchumba wao wa mwisho," Ouma alisema.
Mwili wa marehemu uligunduliwa Jumatatu asubuhi lakini bila majeraha.
Msimamizi huyo alisema wanashuku mwili wa mwanamke huyo ulihamishwa na mpenziwe kutoka alikofia hadi katika boma lingine kwa nia ya kumzika mchangani.
Mshukiwa alikamatwa na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Kipasi kwa uchunguzi zaidi. Familia ya mwanamke huyo ilihakikishiwa haki baada ya kukamatwa kwa mshukiwa.
Mwili wa marehemu ulihamishiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Homa Bay kwa uchunguzi.