Polisi wafunguka sakata la mtoto aliyeibiwa Mwanza

0

 Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linapenda kutoa taarifa kuhusiana na kupatikana kwa mtoto aliyeibwa na tukio la watu wawili kuliwa na mnyama Mamba wilayani Sengerema.

Tarehe 26.03.2023 muda wa saa 08:00 asubuhi, huko mtaa wa Migombani, Kata ya Nyampulukano,Tarafa ya Sengerema, kuliripotiwa taarifa ya wizi wa mtoto aitwaye Anitha Richard mwenye umri wa miezi 6 na mtu ambaye hakujulikana.

Ni kwamba, Mama wa mtoto huyo aitwaye Agnes Robert, Miaka 26, Mkulima, na Mkazi wa Migombani alimuacha mtoto huyo kwa binti yake mdogo aitwaye Martha Richard, Miaka 9 akiwa amembeba mgongoni kisha yeye kuingia bafuni kwa ajili ya kuoga.

Baada ya muda Martha, akiwa amembeba mdogo wake mgongoni aliitwa na jirani yao aitwaye Costancia Deonatus na kumuagiza akiwa na watoto wenzake kufuata ndoo yake kwa mtu aliyekuwa amenunua mkaa kwake ambaye jina lake halikufahamika.

Agnes Robert ambaye ni mama wa mtoto alipomaliza kuoga alitoka na kuanza kuwatafuta watoto wake na ilipofika majira ya saa 13:00 mchana, watoto 02 walirejea nyumbani bila ya yule mwenzao wa miezi 06 aliyekuwa amebebwa mgongoni na dada yake, ndipo wazazi waliweza kugundua kuibiwa kwa mtoto wao na kutoa taarifa kituo cha Polisi.

Baada ya tukio hilo kuripotiwa Askari Polisi walifanya msako mkali na kufika katika kijiji cha Nyamaduke na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa Happyness William, miaka 18, mkulima na mkazi wa Nyehunge akiwa na mtoto huyo aliyetambuliwa na wazazi wake kuwa ndiye aliyeibiwa katika kijiji hicho na baada ya mahojiano ya kina mtuhumiwa amekiri kuhusika na tukio la wizi wa mtoto huyo ambapo alidai kuwa alienda kumuonesha mumewe kuwa amejifungua.

Upelelezi wa kesi hii unakamilishwa mara moja na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo kukabiliana na mkono wa sheria.

Tarehe 24.03.2023 muda wa saa 19:00 jioni huko mwalo wa Kazunzu, kijiji na Kata ya Kazunzu, katika fukwe za ziwa Victoria kuliripotiwa taarifa ya mtu kuliwa na mnyama Mamba. Askari Polisi kwa kushirikiana na wananchi walifika eneo hilo ambapo ndugu waliweza kuutambua mwili wa mtu aliyekamatwa na kuliwa na mnyama Mamba kuwa ni Salome Dotto miaka 30, mkulima na mkazi wa Kazunzu.

Mwili huo umefanyiwa uchunguzi na Daktari na tayari umekabidhiwa kwa ndugu kwa taratibu za mazishi.

Tarehe 09.03.2023 Muda wa saa 13:00 huko kijiji cha Izindabo, kata na tarafa ya Buchosa wilaya ya sengerema, kuliripotiwa taarifa ya mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Primitiva Evarist Miaka 56, Mkulima mkazi wa Izindabo, aliyefariki baada ya kukamatwa na kuliwa na mnyama mamba wakati akinawa miguu katika fukwe za ziwa victoria.

Mwili wa Primitiva Evarist ulitambuliwa na ndugu na kufanyiwa uchunguzi kisha kukabidhiwa kwa taratibu za mazishi.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linaendelea kutoa rai kwa wazazi na walezi kuendelea kuchukua tahadhari na kutimiza jukumu lao la msingi la uangalizi wa watoto na sio kuwaacha peke yao bila uangalizi wa mtu mzima. Aidha, linawaasa wananchi hususani wanaofanya shughuli zao katika fukwe za ziwa Victoria kuchukua tahadhari ya usalama wao wenyewe ili kujiepusha na madhara yanayoweza kujitokeza. Pia, linaomba kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili ziweze kufanyiwa kazi kwa haraka.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 


 

 
#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top