Rais Samia: Nimechoka, sasa hivi mkizingua natimua wote

0

Rais Samia Suluhu Hassan amewaapisha viongozi wakuu wa wizara aliowateua juzi, akitaja sababu ya mabadiliko hayo kuwa ni ugomvi kati yao wizarani, akiwaonya ni mara ya mwisho kuwadekeza.


"Ni jambo ambalo silipendi mtu kutokuelewana, mawaziri na manaibu na makatibu wake, sasa ni mwisho kutumia kupangua mmoja mmoja kwenye wizara. Ikitokea tena, mtaondoka wote kwa pamoja!

"Hili silipendi, sasa ninataka nikiwapanga mfanye kazi, sioni sababu ya kutokuelewana, sizielewi sababu zenu za kutokuelewana," alitamka Rais Samia katika lugha ya ukali, akiorodhesha sababu nyingine nne zilizochangia mabadiliko hayo.

Rais Samia alitoa angalizo maalum kwa Wizara ya Uvuvi na Mifugo, akitamka: "(Waziri Abdallah) Ulega nikuombe sasa ule ugomvi wangu nanyi nenda mkafanye kazi!"

Katika orodha ya sababu hizo, Rais Samia kwenye hotuba yake hiyo jana iliyochukua muda mfupi Ikulu, alitaja sababu nyingine ni kumteua Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Madini, baada ya kubaini kuwapo kusuasua kwa uthibitisho wake, kutoka nafasi ya kukaimu, yeye Rais akiwa ameshaagiza muda mrefu.

Vilevile, akataja sababu ya tatu kuteua wasomi na wenye uelevu, ni kwenda kutumia stadi zao serikalini, pia ni fursa ya kujibu kauli kinzani kutoka nje ya serikali, wahusika hao kushuhudia uhalisi na magumu yaliyomo kwenye nafasi hizo.

"Hakuna Mtanzania asiye na akili, kila mtu mwenye akili tutamchukua na kila mmoja ana akili. Wakiwa nje huko wanazungumza, nao sasa tumewaleta ndani waje watupe ubunifu wao na waone ugumu ulivyo," alitamka Rais katika hotuba yake hiyo, iliyobeba utashi wa kupashana ukweli.

Rais Samia alitaja sababu ya nne inahusiana na maboresho katika mfumo wa kiserikali, jukumu la uwekezaji linahamishiwa ofisini kwake kutoka Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Alifafanua, katika hatua ya kwanza amemteua Katibu Mkuu kuweka mazingira stahiki kabla ya kumteua waziri mwenye dhamana.  Vilevile, vitengo vyake vingine, Tume ya Uwekezaji Tanzania (TIC) na Tume ya Mipango.

"Sekta ya Mifugo na Uvuvi tuone inafanya kazi, kama ulikuwa unafanya ukiwa chini ya mtu, sasa ukafanye na tutaona, nikuombe ukafanye hiyo kazi.

"Niwapongeze manaibu waziri, sio kwamba hamna kosa ila mama analea. Mabadiliko ni kawaida ili kuimarisha serikali na kufikia kasi inayotarajiwa," alisema.

Katika orodha ya walioteuliwa ni: Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega ambaye anakuwa waziri, Hamis Mwinjuma, maarufu Mwana FA, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, akichukua nafasi ya Pauline Gekul aliyehamishiwa Wizara ya Katiba na Sheria.

Baada ya kiapo hicho viongozi hao walikula kiapo cha uadilifu. Rais Samia alifanya mabadiliko madogo kwenye Baraza lake la Mawaziri, makatibu wakuu na wakuu wa mikoa na taasisi za serikali juzi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 

 

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top