Na, Hassan Msellem-Pemba
Alikuwa miongoni mwa wazazi waliokuwa na matumaini makubwa ya kuwa siku moja mtoto wake angemaliza shule na kupata kazi ya ndoto yake.
Hata
wakati akiendelea kufanya uwekezaji ikiwemo kumpatia mahitaji yote ya shule akiwa
kidato cha kwanza, mtoto wake alikatisha masomo na kuacha shule.
Idrissa
Bai Pandu (58), mkaazi wa Chambani Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba
anasema mtoto wake amekatisha masomo baada ya kubakwa, kitendo kilichomuachia
majeraha makubwa ya kisaikolojia.
“Mwanangu alikuwa ana ufahamu mzuri tu
na alikuwa anapenda kusoma na alikuwa ana ndoto nyingi sana ikiwemo kuwa
mwanasheria lakini ndoto hizo zote zimepotea kutokana na kushindwa kuendelea na
masomo baada ya kubakwa kwa nguvu,” anasema
kwa uchungu.
Mara
baada ya binti yake kubakwa, Pandu anasema aliathirika kisaikolojia mpaka kufikia
hatua ya kupata matatizo ya akili na kusababisha ashindwe kuendelea na masomo.
“Kitendo alichofanyiwa kilimfanya kila
anapokutana na watu wengi kujisikia vibaya na kuwa kama mtu aliyechanganyikiwa,” anasema huyo, ambaye matumaini kwa binti yake
kuendelea na masomo anaona kama yamefifia.
Mzee
huyo ni miongoni mwa baadhi ya wazazi visiwani Zanzibar ambao wamekuwa wakikosa
usingizi na kutafuta kila njia ya kuwalinda watoto wao ili wasitumbukie kwenye mikono
ya watu wabaya wakiwemo wabakaji na kutimiza ndoto zao.
Hata
hivyo, juhudi hizo siyo wakati huzaa matunda.
“Mimi kama kiongozi wa familia
nafahamu vyema sana jukumu la kuhakikisha nawalea watoto wangu katika maadili
mema ili kuwalinda dhidi ya vitendo vya ubakwaji lakini unajua kuna mambo mengi
sana yanayosababisha kutokea kwa vitendo hivyo,”anasema Ali Omar Juma, mkazi wa Chake Chake.
“Miongoni mwa hivyo ni marafiki
wabaya, matumizi mabaya ya simu pamoja na vishawishi ukiachana na wale ambao
wanabakwa kwa kutumia nguvu,” anasema
Juma
(67).
Juma,
baba wa watoto anasema licha ya wazazi kutimiza wajibu wao, mazingira wanayokuwepo
watoto nje ya nyumbani huchangia kufanyiwa ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji
kwa watoto wa kike.
Ubakaji
umekuwa ukihusishwa pia na imani za kishirikina, ukosefu wa maadili na kushamiri
kwa makundi rika yanayochochewa na matumizi ya dawa za kulevya.
Hata
hivyo, Sheria ya Watoto ya Zanzibar ya mwaka 2011 inasisitiza jamii na wazazi wazazi
na jamii kubeba jukumu la kumlinda na kila hatari ikiwemo vitendo vya uzalilishaji
vinavyorudisha nyuma ustawi na ukuaji wake.
HALI ILIVYO ZANZIBAR.
Kwa
mujibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Tawi la Pemba
na Jumuiya ya Tumaini Jipya Pemba (TUJIPE), matukio 88 ya ubakaji yaliripotiwa
mwaka 2022 kutoka 44 ya mwaka juzi
Chake
Chake.
Hiyo
ni sawa na kusema ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, matukio ya ubakaji
yaliongezeka kwa asilimia 50, kasi ambayo ni kubwa hasa kwa mstakabali wa mtoto
wa kike.
Tatizo
la ubakaji siyo la Chake Chake pekee, bali linasumbua katika maeneo mengine ya
Zanzibar.
Ofisi
ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS) inaeleza kuwa matukio ya ubakaji
Zanzibar yameongezeka kutoka matukio 1,222 mwaka 2021 hadi matukio 1,360 mwaka
2022.
Hilo
ni ongezeko la matukio 138 (asilimia 11.3) ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
Katika
kupambana na vitendo vya ubakaji nchini viongozi wa dini nao wanajukumu kubwa
la kuhakikisha vitendo hivyo vitokomezwa.
Lakini
je, wanafahamu dhima na wajibu wao katika jamii katika kuielimisha jamii ili kukabiliana
na vitendo vya ubakaji?
Naibu
Katibu kutoka Ofisi ya Mufti Mkuu kisiwani Pemba, Sheikh Said Ahmad Mohammed
anasema wamekuwa na utaratibu wa kutoa mafunzo juu ya vitendo vya ubakiji kwa
walimu wa madrasa kila baada ya miezi mitatu ili kuhakikisha wanapata elimu
hiyo kusudi waweze kuitoa kwa wanafunzi.
Pia
wana programu za kutoa elimu ya kupambana na vitendo vya ubakaji kwa wananchi katika
maeneo wanayoishi pamoja na vyombo vya habari.
“Kiujumla Ofisi ya Mufti Kisiwani
Pemba imeandaa programu nyingi sana katika kupambana na vitendo vya ubakaji,
miongoni mwa program hizo ni kutoa mafunzo kwa walimu wa madrasa, kupita
mitaani pamoja na kutumia vyombo vya habari kuhakikisha wananchi wanapata
uelewa wa kutosha kupambana na vitendo vya ubakaji,” anasema Sheikh Mohammed.
Licha
ya walimu wa madrasa kutakiwa kuwa mfano wa kuigwa, baadhi yao wamekuwa wakishiriki
vitendo hivyo kikatili kwa watoto wa kike.
Kwa
mujibu wa Ofisi ya Mufti Mkuu Kisiwani Pemba, walimu wa madrasa saba wametuhumiwa
kwa vitendo vya ubakaji mwaka 2022, ambapo walimu 3 kati ya hao walikutwa na
hatia na kuhukumiwa kutumikia vifungo mbalimbali.
MAHAKAMA NAYO YATIMIZA WAJIBU WAKE.
Kwa
mujibu wa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali Mkoa wa Kusini Pemba, kesi 128
za ubakaji zilifikishwa Mahakama ya Mkoa Chake Chake mwaka jana. Kati ya kesi hizo,
97 zilitolewa hukumu na kesi 56 washtakiwa walikutwa na hatia na kuhukumiwa kutumikia
vifungo pamoja na kulipa fidia.
“Kwa mujibu wa takwimu tulizonazo
ukiangalia mwaka 2022 idadi ya matukio ya ubakaji kwa wanafunzi yamekuwa mengi
zaidi kuliko mwaka 2021, ambapo takwimu zetu zinaonyesha takriban kesi 128
ziliripotiwa katika mahakama yetu ikilinganisha na mwaka jana ambapo kulikuwa
na kesi 88,
“Hivyo hii inadhihirisha kuwa bado
suala la ubakaji ni donda ndugu katika visiwa vyetu vya Zanzibar licha ya
Mheshimiwa Rais wa Zanzibar kuanzisha mahakama maalum ya kupambana na makosa
udhalilishaji,” anasema
Mwendesha Mashtaka wa Serikali Ali Amour
Makame.
Mratibu
wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Pemba, Fat-hia Mussa
Said suala la ubakaji siyo la kufumbiwa macho na kila mtu anawajibika kukabiliana
nalo.
“Sisi
kama wanaharakati wa kupambana na vitendo vya udhalilishaji ikiwemo ubakaji tumekuwa
tukifanya programu mbalimbali ikiwemo kukutana na wadau, waandishi wa habari,
walimu wa madrasa, viongozi wa dini, vipeperushi, kampeni mbalimbali, makongamano
na mijadala ili kuhakikisha wananchi wanapata uelewa katika
kukabiliana
na vitendo hivyo.
“Kwa kiasi fulani tunasema tumepiga
hatua kwa sababu licha ya kuona matukio ya ubakaji yameongezeka lakini hiyo
imetokana na wanachi kutoa taarifa pindi yanapotokea matukio ya ubakaji
sambamba na vyombo vya habari kuripoti matukio hayo,” anasema Fat-hia.