Hatmaye kilio cha miaka mingi cha kukosa nishati ya umeme kwa wakazi wa kijiji cha Mfereke kata ya Utalingolo halmashauri ya mji wa Njombe mkoani Njombe kimeanza kupungua baada ya serikali kufikisha umeme kwa mara ya kwanza kijijini hapo.
Kwa hatua ya awali umeme huo umefikishwa katika kanisa la Roman catholiki Mfereke ambapo baadhi ya wananchi wa kijiji hicho akiwemo Walter Mwanyika,Juliana Mlowe na Flouris Mwanyika wameshukuru kwa hatua hiyo huku wakihoji masuala mbalimbali pamoja na kuomba umeme huo kupelekwa kwa wananchi.
Diwani wa Kata ya Utalingolo Erasto Mpete ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Njombe anatumia fursa hiyo kuwataka wananchi kwenda kunufaika kimaendeleo kupitia nishati hiyo huku akimshukuru Rais kwa hatua hiyo pamoja na Mbunge Deo Mwanyika.
Maofisa kutoka shirika la Umeme Tanzania Tanesco mkoa wa Njombe wamefika kutoa elimu kwa wananchi juu ya Matumizi ya umeme huo ambapo Mhandisi mkuu wa Mkoa Meshack Laurent na Desmond Komba Wanabainisha Faida na hasara za umeme pindi utakapowafikia hadi majumbani mwao na kwamba wanapaswa kuwa makini na matumizi yake na kulinda miundombinu yake.
Kwa upande wake afisa uhusiano wa Tanesco mkoa wa Njombe Neema Lyakurwa anawataka wananchi wa Mfereke kuwa makini na vishoka watakaowafuata kutaka kuwaunganishia umeme ndani ya nyumba zao kwani wanaweza kuwaibia na wasipate pakukimbilia.
Kijiji cha Mfereke kilichopo umbali wa takribani Km 6 toka mjini Njombe kilikosa umeme kwa miaka mingi ilihali vijiji vingine vya kata ya Utalingolo kikiwemo Utalingolo yenyewe kilipata nishati hiyo kipindi kirefu.