Auawa akigombea maji ya kupikia

0

 Mkazi mmoja wa Kijiji cha Vuo, Wilaya ya Mkinga, Amiri Mohamed (24) ameuawa kwa kuchomwa na kisu baada ya kutokea ugomvi wa kugombea maji ya kupikia.

Picha kutoka maktaba haihusiani na tukio halisi

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Henry Mwaibambe ni kuwa mauaji hayo yalifanyika jana saa 4 asubuhi katika Kitongoji cha Vuo, Kata ya Vuo wilayani hapa.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema vijana hao licha ya kwamba ni waumini wa dini ya Kiislamu hawana kawaida ya kufunga. Hivyo unapofikia mchana huenda katika kibanda kilichojificha na kujipikia vyakula kisha kula mchana kwa tahadhari ya kuonekana na waliofunga Ramadhani.

"Hakane Nyundo alimfuata mwenzake Amiri na kumtaka ampe maji yaliyokuwa kwenye ndoo ili apikie, lakini Amiri alipokataa, wakashikana. Alipoona anazidiwa nguvu akaenda kuchukua kisu na kumchoma," amesema Husna Hamad.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kitongoji, Mohamed Kunema alisema baada ya kuchomwa kisu kwenye ubavu wa kushoto, uongozi ulimuwahisha Kituo cha Afya cha Kiwengu ambako waliamua kumpa rufaa ya kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga ya Bombo lakini alifariki njiani.

"Hawa vijana hawana kawaida ya kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhani huamua kwenda kwenye mageto kujipikia na kula mchana kwa kificho...Sijui ilikuwaje Nyundo alipoona amezidiwa akaamua kumchoma kisu mwezie," amesema Mwenyekiti.

Akithibitisha habari hizi, Kamanda Mwaibambe amesema Hassan Nyundo anashikiliwa na polisi, baada ya uchunguzi kukamilika atafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Sheikh wa Mkoa wa Tanga, Juma Luwuchu alisema kwa mujibu wa maelekezo. Hassan na Amiri walikuwa wamefikisha umri wa kisheria wa kufunga Ramadhani kwa sababu anayefika miaka 18 anahukumiwa kutenda dhambi asipotekeleza agizo la kufunga.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 


 

 
#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top