Baba ajinyonga chumbani kwa watoto baada ya kuchoka kuumwa

0

 Aden Mwakipesile (49) mkazi wa Kijiji cha Ibindi, Wilaya ya Mpanda amejinyonga kwa kutumia kamba ya katani chumbani kwa watoto wake, kwa kile kinachodaiwa kuwa alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa mshipa wa ngiri kwa muda mrefu.

Picha kutoka Maktaba

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Aprili 4, 2023 kijijini hapo, baada ya mke wake Leticia Deus kusinzia kisha, mgonjwa huyo alikwenda chumbani kwa watoto na kujinyonga.

“Alikuwa anaumwa mshipa wa ngiri kwa muda mrefu, jana alijisikia maumivu muda wa jioni. Ilipofika usiku aliniambia nimkorogee uji, akanywa,” amesema.

“Tukaenda kulala lakini nikasinzia. Sifahamu aliamka saa ngapi, asubuhi sikumkuta kitandani nikajua atakuwa ametoka nje,” ameeleza mke wa marehemu.

Amesema asubuhi wakati anafagia nje kwenye chumba cha watoto cha nje akaona mlango wazi alipoingia akamkuta amejining’iniza na kamba ya katani.

“Sijui chochote, alikuwa hajaniambia. Nadhani alichooka na ugonjwa akaamua kujinyonga, ameniachia watoto wawili na huku alihamia tu nyumbani kwao ni Mbeya,” amesema.

Baadhi ya mashuhuda wamesikitishwa na kitendo hicho wakimzungumzia marehemu kuwa alikuwa mtu mwema, huku wakiisihi jamii inapokumbwa na matatizo ishirikishe wengine.

Christopha Modest jirani wa marehemu amesema jioni alizungumza naye akiomba ampatie dawa ya ugonjwa uliokuwa unamsumbua.

“Nilimsihi avumilie niitafute dawa nitampatia maana niliyokuwa nayo nilimpa mtu mwingine, ajabu napigiwa simu asubuhi amejinyonga,”amesema Modest.

Jirani mwingine wa marehemu Mwamvua Mabula amesema alikuwa anaishi na watu vizuri huku akitoa rai kwa wanandoa kuwa na subira wanapokumbwa na matatizo.

Diwani wa Kata ya Ibindi, Daniel Itangu amekiri kuwepo tukio hilo akitoa rai kwa wanandoa kuvumilia changamoto za maisha ikiwamo maradhi.

“Nimesikitika sana baada ya kupata taarifa hizo jana nimesalimiana naye vizuri, alikuja Ibindi akiwa mtoto amekulia hapa nimecheza naye japo mie ni mkubwa kwake,” amesema.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 


 

 




#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top