Bweni lateketea kwa moto Arusha leo

0

Bweni la wavulana wa Shule yenye mchepuo wa kiingereza ya Green Valley iliyopo jijini Arusha,limeteketea kwa moto asubuhi ya leo na kupelekea uharibifu mkubwa wa mali za wanafunzi na shule, huku wanafunzi zaidi ya 15 wakinusurika.


Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi wa shule hiyo, Yahaya Njarita alisema hakuna mwanafunzi aliyedhurika na janga hilo la moto zaidi ya vifaa vyao vya shule vilivyoteketea na baadhi kuokolewa.

Alisema bweni hilo lilianza kuteketea majira ya saa nne asubuhi huku chanzo cha moto huo kikiwa bado hakijajulikana na uchunguzi wa jeshi la polisi unaendelea.

Kwa mujibu wa maelezo ya mashuhuda wa tukio hilo wamesema waliona moshi ukitoka katika moja ya vyumba katika bweni hilo na kupiga kelele zilizosaidia wanafunzi kujikusanya kwa kushirikiana na wafanyakazi na kuanza jitihada za kuzima moto huo.

"Unajua shule yetu huwa tunatoa mafunzo ya kuzima moto hivyo baada ya kuwepo kwa taarifa hiyo moja kwa moja wanafunzi kwa kushirikiana na majirani tulianza kuzima na baadaye jeshi la zima moto na uokozi walifika na kufanikisha kuzima moto huo "

Aidha, Njarita alisisitiza kuwa hakuna mwanafunzi yeyote aliyepata madhara ya moto na wapo salama ila hasara ni kubwa ya mali na vifaa vya wanafunzi kuteketea.

Alisema bweni hilo lenye vyumba vitatu, wanafunzi wanaolala huwa ni 75 ila waliokuwa wameripoti baada ya shule kufunguliwa leo ni 15 ambao hata hivyo wakati moto ulipozuka walikuwa darasani.

Kwa upande wake Mrakibu wa jeshi la zima moto na uokozi na kamanda wa mkoa wa Arusha , Osward Mwanjejele alisema kuwa jeshi hilo lilipokea taarifa ya wito wa tukio hilo majira ya saa 4.54 asubuhi na kufika eneo la tukio wakati moto ukiendelea kuwaka kwa kasi kubwa.

Alisema walifanikiwa kuzima moto huo huku sehemu kubwa ya jengo na mali za wanafunzi zikiteketea kwa sababu ya mazingira magumu ya kuzima moto kutokana na ufinyu wa eneo.

"Tulifanikiwa kuzima moto na kuokoa chumba kimoja huku vyumba viwili vikiteketea hii ni kutokana na jengo hilo kutokuwa na sehemu ya kupita kirahisi upande wa nyuma"alisema

Alisema chanzo cha moto huenda ikawa hitilafu ya umeme kwa sababu jengo hilo linaonekana kuwa la zamani na kutofanyiwa marekebisho ya mfumo wa nyaya za umeme.

"Taarifa za awali zinaonesha moto ulianzia juu ya dari na hii inawez kuwa ni hitilafu ya umeme iwapo kama mfumo wa waya za umeme hujafanyiwa marekebisho kwa muda mrefu kwani sheria za zima moto zinataka mfumo wa waya za umeme ufanyiwe marekebisho kila baada ya miaka 15"alisema

Baadhi ya wazazi waliosikia tukio hilo na kufika , Joseph Emmanuel na Agness Amos walisema kuwa walipata mshtukio mkubwa na kuzimia ila wanashukuru mungu baada ya kufika eneo la tukio wakikuta watoto wao wapo salama japo vifaa vyao vimeteketea .

"Niliposikia bweni linaungua na moto na mimi ndo mtoto wangu nilimpeleka shuleni leo asubuhi nilipata hofu na kuzimia ila nilipofika shuleni nilikuta mwanangu yupo salama ila vitu vyake ndio vilikuwa vimeungua," alisema Agnes.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 


 

 
#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top