Tukio la kusikitisha na kushangaa limeibua simanzi baada ya dada wawili kukatisha uhai wa kaka yao ambaye jina lake halikutajwa kwa kumshushia kipigo wakati alipoulizia chakula.
Tukio hilo lilitokea Jumanne ya Machi 28 usiku katika kaunti ya Bungoma nchini Kenya ambapo kijana huyo alirudi nyumbani usiku na kuulizia chakula ndipo alikumbana na kipigo hicho kilichomsababishia umauti.
Baba yake mzazi aitwaye Shadrack Mukoyani amesema kuwa wakati wa purukushani kati yao dada yake mmoja alichukua ukuni akampiga nao kichwani na kufariki papo hapo.
Akithibitisha kisa hicho, Kamanda wa Polisi wa Webuye Mashariki, Irene Kerubo amesema kuwa siku hiyo, marehemu ambaye hakuwa ameoa, alirejea nyumbani usiku wa saa tano akawa anaulizia chakula kutoka kwa dada zake hao.
Kerubo amesema baada ya kuagiza chakula huenda ndio kisa cha dada zake kukasirika na kuanza kumshushia kipigo. Polisi wamesema wanaendelea na uchunguzi zaidi juu ya mauaji hayo.