Wazazi na walezi wenye watoto yatima wametakiwa kuongeza umakini wa kuwa karibu na watoto wao ili kuwaepusha na vitendo vya udhalilishaji.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa zoezi la ugawaji wa vyakula huko katika ukumbi wa Umoja ni Nguvu Hall Mkoani, Makamo mwenyewekiti wa jumuiya ya Faraja Yetu Bi. Riziki Mohammed Ramadhan, amesema kutokana kukithiri kwa vitendo vya udhalilishaji nchini Wazazi na walezi wanapaswa kuongeza umakini wa kuwa karibu na watoto ili kuwaepusha na vitendo hivyo.
Amesema "Kama tunavyojua saa hizi kuwa tumekumbwa na janga la udhalilishaji kina Kona udhalilishaji udhalilishaji sio watoto wa kike Wala wakiume kwahivyo niwaombe sana wazazi wenzangu na walezi tuweni Makini sana na Watoto hususan hawa watoto yatima ndio ambao wamekuwa wahanga wakubwa wa vitendo vya udhalilishaji kwani wanaofanya vitendo hivyo wanatambua kuwa Hawa watoto hawana baba wengine hawana hata mzazi mmoja kwahivyo wanajua wakiwadhalilisha hawana watu ambao wataweza kuwashughulikia ipaswavyo katika Ufuatiliaji wa kesi"
Kwa upande wake mjumbe wa Jumuiya ya Faraja Yetu Suleiman Mahmoud Muhammad, amesema suala la kuzisaidia familia zenye watoto yatima ni jukumu la kila mmoja ili familia hizo ziweze kujikimu kimaisha hususan katika kipindi hichi cha mwezi mtukufu wa Ramadhan.
"Suala la kuzisaidia familia zenye watoto yatima sio suala la mtu mmoja au taasisi Moja peke yake, hili suala la Kila mmoja kwani watoto yatima ni wetu sote hata Mtoto wako ambaye Leo ana baba na Mama kesho anaweza kuwa Mtoto yatima, hivyo basi hatuna budi kujitoa Kila mmoja kwa nafasi yake kuzisaidia familia hizi ili nazo zipate faraja napia nao wajihisi kuwa Wana haki sawa na Watoto ambao sio yatima katika jamii zetu"
Nao baadhi ya wazazi na walezi wenye watoto yatima waliopatiwa msaada huo wameishukuru jumuiya hiyo sambamba na kuziomba Jumuiya nyengine kuiga mfano huo.
Yusuf Khamis Silima Mkaazi wa Kangani ambaye ni miongoni mwa wazazi wenye watoto yatima ameishukuru jumuiya ya Faraja Yetu katika kujitoa kwake katika kuzisaidia familia zinazoishi katika mazingira magumu ili nazo ziweze kupata faraja katika kipindi hichi cha mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Jumla ya familia 120 zenye watoto yatima 303 kutoka Unguja na Pemba zimepatiwa msaada huo wa vyakula uliojumuisha mchele kilo 10, Unga kilo 5, Sukari kilo5 na mafuta ya kupikia lita 1, ambao umetolewa Jumuiya ya Faraja Yetu.