Mkutano wa 11 wa Bunge la 12 ambao ni mahususi kwa bajeti ya serikali 2023/24, unaingia juma la nne ambalo pamoja na mambo mengine, hatima ya mchakato wa Katiba mpya inatarajiwa kujulikana.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Bunge, wiki hii wabunge watajadili makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais - Muungano na Mazingira, Wizara ya Madini na Wizara ya Katiba na Sheria.
Miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kupatiwa ufafanuzi na Wizara ya Katiba na Sheria ni kukwamua mchakato Katiba mpya pamoja na marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa na ya uchaguzi.
Hivi karibuni, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro, akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo jijini hapa, alisema mchakato wa Katiba mpya unatarajiwa kuanza kufanyiwa kazi baada ya kupitishwa kwa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2023/24.
“Mchakato wa Katiba mpya ni agizo la Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo ili kufanikiwa, mchakato wake unahitaji rasilimali fedha nyingi na wajumbe wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi mtambue mna jukumu hilo la kupitia mapendekezo ya bajeti ya mwaka huu 2023/24 kufanikisha mambo hayo makubwa ya kitaifa," alisema.
Dk. Ndumbaro alisema hitaji la Katiba mpya ni la watanzania, hivyo wizara yake inatakiwa kujipanga kuhakikisha inakamilisha mchakato huo kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwakani na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
"Marekebisho ya sheria za uchaguzi huo yanahitajika pamoja na Sheria ya Tume ya Uchaguzi, hivyo wizara yetu inahitaji rasilimali fedha kupitishwa ili kukamilisha michakato hiyo haraka," alisema.