Hatua za kuchukuliwa kunusuru kutoweka kwa mikoko Zanzibar.

Hassan Msellem
0

 Na, Hassan Msellem, Pemba

Mwambe lilikuwa ni eneo lenye mikoko mingi, iliyonawiri kwa rangi ya kijani ambayo ilimvutia kila anayepita katika eneo hilo.


Sasa, hali ni tofauti. Eneo hilo limekuwa kama jangwa. Kwa wageni wanaofika hawawezi kujua kama Mwambe ilikuwa miongoni mwa maeneo muhimu yenye uoto wa asili ambao ulikuwa ukichangia kuhifadhi mazingira.

Uvamizi wa wananchi ambao walikuwa wakikata mikoko, ndiyo umebadilisha sura ya eneo hilo.

 

Ni eneo lililoko ukanda wa bahari ya Hindi mwa Kisiwa cha Pemba, Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba, Shehia ya Mwambe, ambalo wananchi walilitumia kama sehemu ya kitega uchumi chao.

 

Walikuwa wanakata mikoko mikubwa na midogo kwa ajili ya kuni, ujenzi na upigaji mkaa pasipo kujua au kwa kujua kuwa vitendo hivyo vimechangiwa kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira na kulifanya eneo hilo kuwa katika hatari kubwa ya kukumbwa na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo mafuriko na ukosefu wa mvua.

 

Ali Khamis Seif, mkaazi wa Mwambe anayejishughulisha na shughuli za upigaji wa mkaa kwa kutumia miti ya mikoko anasema licha ya kufahamu athari za ukataji wa mikoko lakini wanalazimika kufanya shughuli hiyo ili kupata fedha za kujikimu.

 


“Tunafahamu kuwa athari zipo maana ndio kama hivi kwa sasa eneo hili ambalo lilikuwa limezongwa na mikoko limekuwa jangwa na maji yanapanda juu kwa kasi hadi kufikia kuingia mashambani lakini tunajikuta tunalazimika kukata mikoko kwa ajili ya kupata kuni, kujengea na kupiga mkaa ili tupate kujikimu,” anasema Seif (42).

Hali siyo njema

Afisa Mazingira kutoka Idara ya Misitu kisiwani Pemba, Ali Abdi Juma anasema jumla ya maeneo 12 Pemba yameathirika kutokana na ukataji wa miti hususan mikoko kwa shughuli za upigaji wa mkaa na ujenzi.

 

Takwimu za idara hiyo ya misitu zinaonyesha kuwa asilimia 70.8 ya eneo lote la Mwambe lenye ukubwa wa ekari 1,552 limekuwa kama jangwa. Mikoko 928,203 imekatwa katika kipindi cha miaka mitatu (2020 hadi 2022).

 

Siyo Mwambe pekee. Maeneo mengine ambayo yameathirika kwa ukataji wa mikoko Pemba ni pamoja na Kengaje, Vitongoji, Chokocho, Wambaa, Shumba, Tumbe, Mnarani, Wingwi, Kichuuani, Tundaua na Msuka.

 

Pia takwimu zinaeleza zaidi kuwa asilimia 44.3 ya maeneo 12 kati ya 35 yenye mikoko katika Kisiwa cha Pemba yameathirika vibaya na ukataji wa mikoko.

 

Tatizo la ukataji wa mikoko ni Zanzibar yote.

 

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar inayoshughulikia mazingira na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) zinaonesha jumla ya maeneo yenye mikoko 68 Unguja na Pemba yamekumbwa na tatizo la ukataji wa kiwango cha juu cha miti hiyo.

 

Zaidi ya mikoko milioni 964.9 imekatwa kati ya mwaka 2020 na 2022.

Ripoti ya Hali ya Mikoko Duniani kwa mwaka 2022 iliyotolewa na Muungano wa Mashirika Yanayosimamia Mikoko Duniani (GMA) inaeleza kuwa kilomita za mraba 147,000 za mikoko ndio zimebaki duniani kote kwa sasa.

Eneo hilo la mikoko iliyobaki ni sawa na ukubwa wa nchi ya Bangladesh huku ikieleza kuwa kilomita za mraba 5,245 za miti hiyo zimetoweka tangu mwaka 1996 ikichagizwa na shughuli za kibinadamu.

 


GMA inakusudia kurejesha eneo la kilomita za mraba 8,183 lenye mikoko ifikapo 2030 hasa katika nchi za Asia, jambo litakalosaidia kupunguza athari za uharibifu wa mali unaotokana na dhoruba na upepo wa bahari.

 

Ripoti  ya Hali ya Mazingira Zanzibar ya mwaka 2021 iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais inaeleza kuwa Zanzibar ina hekta 16,488 za misitu ya mikoko sawa na asilimia 9.1 ya hekta 181,536.38 misitu nchini humo.

Ripoti ya Sensa ya Misitu ya mwaka 2013 inaonesha kuwa ukataji na upoteaji wa misitu Zanzibar upo kwa wastani wa asilimia 1.2 ya kiwango cha misitu kilichopo, hiyo ni sawa na hekta 1,277 kwa mwaka.

Shirika lisilo kuwa la kiserikali la 2 Winds linalojishughulisha na utunzaji na uokoaji wa mikoko Zanzibar, linaeleza kuwa miti hiyo ina faida nyingi ikiwemo kutengeneza mpaka kati ya bahari na nchi kavu, inapunguza athari za upepo na mawimbi ya bahari kufika nchi kavu na inasaidia kupunguza uzalishaji wa gesi ukaa.

 

Shirika hilo linaeleza kuwa ongezeko la idadi ya watu, ukataji wa miti kwa ajili ya kuni, mkaa na uendelezaji wa fukwe kwa ajili ya shughuli za utalii ni miongoni mwa sababu zinazochangia kasi ya kupotea miti hiyo.

Sababu nyingine ni utupaji hovyo wa taka na uchafuzi wa bahari.

 

Athari za ukataji ovyo wa mikoko

Afisa Tathmini na Utunzaji wa Misitu kutoka Idara ya Misitu Pemba, Ali Zubeir Juma anasema miongoni mwa athari za ukataji wa mikoko ni kuwepo kwa jangwa na kuruhusu kiwango cha bahari kuvamia maeneo ya nchi kavu kwa urahisi.

 

“Kwa kweli kuna athari nyingi sana za ukataji wa mikoko ikiwemo kuyafanya maeneo yenye mikoko kuwa jangwa, lakini kuruhusu kiwango cha bahari kuvamia maeneo ya nchi kavu kwa kasi zaidi kutokana na kukosekana kwa kizuizi cha maji ya bahari kuingia nchi kavu,” anasema Juma.

 

Hatua zinazochukuliwa

Afisa Tathmini na Utunzaji wa Misitu kutoka Idara ya Misitu Pemba, Ali Zubeir Juma anasema wameandaa mpango mkakati na ‘kampeni ya tunza mikoko kwa maslahi yako’ ambayo ilianza kutekelezwa mwaka 2020 na jumla ya maeneo nane ambayo yalikuwa yameathiriwa vibaya kwa ukatwaji wa mikoko imerudishwa katika hali yake ya kawaida.

 

“Kuna hatua mbalimbali ambazo tunazichukua kwa wananchi ambao tunawashika kwa makosa ya uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji wa mikoko na kuanzia Januari hadi Desemba 2022 jumla ya wananchi 47 tumewatoza faini na kuwapa adhabu ya kupanda mikoko katika maeneo ambayo yameathirika hatua ambazo zinaonekana kuleta tija,” anasema Juma.

 

 

Nasim Juma Shoka ni Mwendesha Mashtaka wa Serikali kutoka Mahakama ya Mwanzo Kengaja, anasema kati ya Machi 2020 hadi Novemba 2022 jumla ya mashauri 68 yanayohusu uharibifu wa mazingira yamesomwa katika mahakama hiyo na mashauri 42 kati ya hayo washtakiwa wamekutwa na hatia na kutozwa fidia kulingana na makosa yao.

“Mashauri mengi yanahusiana na uharibifu wa mikoko Mkoa wa Kusini Pemba na jumla ya mashauri 42 kati ya hayo tayari tumeyatolea maamuzi ikiwemo washtakiwa kutozwa faini,” anasema Shoka.

 

Pia miongozo ya sera na sheria, mfumo wa kitaasisi juu ya mabadiliko ya tabianchi, kuzindua mkakati wa mabadiliko ya tabianchi ni hatua nyingine zinazochukuliwa kudhibiti tabia ya ukataji mikoko.

 

Hatua nyingine ni ujenzi wa kuta za kuzuia mmomonyoko wa fukwe pamoja na kupanda kwa maji ya bahari katika maeneo ya kilimo.

 

Kuta hizo zimejengwa eneo lililopandwa Mikoko katika eneo la Kisakasaka na Kilimani zenye jumla ya urefu wa mita 420, Kisiwa Panza (mita 50), Msuka ujenzi unaendelea (mita 500) na Mizingani - Forodhani mita 308.

 

Kufanyiwa mapitio Mkakati wa Mabadiliko ya Tabianchi (Climate Change Strategy) pamoja na Mpango Kazi wake katika muktadha wa vipaumbele vipya vya Dira ya 2050 na uchumi wa buluu navyo vitasaidia kukabiliana na kutoweka kwa mikoko.

 

Zanzibar ilifanya mapitio ya Sera ya Mazingira ya mwaka 1992 na kuzindua Sera mpya ya Mazingira ya mwaka 2013, ambayo lengo lake kubwa ni kutoa mwongozo juu ya usimamizi bora wa masuala ya kimazingira.

 

Sera hiyo ilitayarishwa kutokana na mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii yanayosababisha matumizi makubwa ya maliasili zilizopo na kuongeza shinikizo kubwa kwenye mifumo ya ikolojia iliyopo baharini na ardhini/nchi kavu sambamba na kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi.

 

Zanzibar inapokea Dola za Marelkani 200 (Sh468,000) hadi Dola 900 (Sh2.1 milioni) kwa hekari kutoka UNDP kwa Wazanzibari hususan wale waliopo katika jamii za pwani kutokana na uhusiano wa karibu na utegemezi juu ya mikoko kwa maisha na chakula na kulinda kina cha bahari kupanda nchi kavu.

 

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mazingira katika ripoti yake ya  hali ya mazingira Zanzibar ya mwaka 2021 inaeleza kuwa kutokana na shughuli hizo katika kipindi cha mwaka 2016 hadi 2021, wastani wa hekta 233.5 za mikoko zimepandwa na zinatunzwa Unguja na Pemba na Asasi za Kiraia Zanzibar.

 

“Sambamba na hayo, pia wapo baadhi ya wananchi ambao wanapenda mazingira ambao wameshiriki katika kupanda, kutunza na wanamiliki kiwango kikubwa cha hekta za miti,” inaeleza ripoti hiyo.

 

 

 

 

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 


 

 
#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top