Chrisma Lete ambaye ni katekista wa kanisa la Roman Catholic kigango cha Igombola,Lupembe halmashauri ya wilaya ya Njombe anatajwa kukimbia kijiji mara baada ya kuhusishwa kwenye tuhuma za kujihusisha kimapenzi na kumpa mimba mwanafunzi wa kidato cha kwanza wilayani humo.
Amos Mwashambo ni mtendaji wa kijiji cha Igombola amethibitisha juu ya tuhuma zinazomkabili katekista ambapo amesema mara baada ya Katekista kusikia ametajwa kuhusika na kitendo cha kumpa ujauzito mwanafunzi aliyekuwa akisoma shule ya sekondari Kidegyembe ndipo alipoamua kutoroka.
"Baada ya huyu binti kufikishwa Polisi ndipo alipotaja kuwa katekista ndio amehusika na hili swala japo awali alimtaja kijana mmoja anayefanya kazi mashambani ambaye alikataa na kudai kuwa yeye alimtongoza tu huyu mwanafunzi lakini hakulala nae,Kwa hiyo inaonekana Katekista alipata upepo kuwa anatafutwa ndio akaondoka"amesema Mwashambo
Kaka wa mwanafunzi ambaye aliomba kuto tajwa jina lake amesikitishwa na kitendo cha ndugu yake kusitishwa masomo na wanaume wasio kuwa na huruma huku akiziomba mamlaka kuchukua hatua kali za kisheria kwa kuwa ndugu yake amerejeshwa nyumbani kuendelea kulea ujauzito unaokadiliwa kuwa na miezi miwili.
Mkuu dawati la jinsia na watoto mkoa wa Njombe Wilfred Willa amekiri kupokea taarifa hiyo ambapo tayari file la kumtafuta na kumkamata mtuhumiwa lipo mikononi mwa Polisi huku akibainisha kuwa mara baada ya mtuhumiwa kukamatwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe atatoa ufafanuzi."File lipo tuliipata taarifa na tunaendelea kumtafuta"alisema Willa
C&P-Uplandsfm