Mkurugenzi wa uzalishaji kutoka wakala wa Mbegu ASA Dkt. Justin Ringo amewapongeza wakulima wa Ngano Makete kwa kuchangamkia fursa ya Kilimo cha zao hilo.
Ametoa pongezi hizo Aprili 19, 2023 akiwa katika zoezi la ufuatiliaji kwenye mashamba ya Wakulima, Taasisi na wawekezaji katika Kata ya Lupalilo, Mang’oto na Mbalatse
Dkt. Ringo amesema hali ya mashamba ya wakulima na wawekezaji wa Ngano inaridhisha na kuwapongeza wakulima hao kwa kuitikia wito wa Viongozi wao ngazi ya Halmashauri na Mkoa wa kuhamasisha Kilimo cha Ngano ambacho kinaweza kuwa mkombozi mkubwa kiuchumi kwa WanaMakete.
Ameongeza kuwa Serikali ipo tayari kuongeza Mbegu kwa wakulima mwaka ujao kwenye msimu wa Kilimo na kuongeza kuwa pembejeo muhimu kwa ajili ya zao hilo zitakuwa zikipatikana karibu na wakulima.
Aniseth Ndunguru Afisa Kilimo Wilaya ya Makete amesema Zaidi ya ekari 200 zimelimwa na Wawekezaji, Wakulima, na vikundi vya Vijana maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Makete huku akiongeza kuwa Halmashauri imeweka mkakati wa kuifanya Makete kuwa eneo la uzalishaji wa Ngano nchini na kuipongeza Serikali chini ya Wizara ya Kilimo kwa usimamizi wa Kilimo na kutambua thamani ya Mkulima hususani wakulima wa Makete.
Kayanda Chengula, Francisca Chaula na Saney Sanga ni miongoni mwa wakulima waliotembelewa na wataalamu wa Kilimo kutoka ASA na ngazi ya Halmashauri ya Wilaya ya Makete wameishukuru Serikali kufuatia kugawa mbegu aina ya SIFA ambazo zimestawi vizuri na kuwapongeza wataalamu wa Kilimo kwa kuwatembelea mashambani na kuwashauri mara kwa mara na kuwapa mbinu za utunzaji wa zao hilo.