Familia moja mtaani Kibra imebaki kwa majonzi baada ya kumpoteza mtoto wao wa miezi minne kwenye makabiliano ya polisi na waandamanaji.
Kwa mujibu wa familia hiyo, polisi walituba gesi ya kutoa machozi kwa waandamanaji na kuingia katika nyumba yao.
Ni gesi ambayo iliishia kilio kwa wao na sasa hawatawahi kumuona mtoto wao wa miezi minne ambaye alizidiwa na kufariki dunia.
Jos Kemunto alisema yeye hakuwa kwenye maandamano ila sasa anaumia moyoni pakubwa baada ya kumpoteza mtoto wake Precious Mong'ina.
Ukali wa gesi hiyo ulimzidia mtoto huyo na mamake anasema alikuwa akijaribu kutuliza hali kwa kutumia kitambaa chenye unyevu wa maji.
Hata hivyo, mtoto Precious aliendelea kulia kutokana na kile mamake anasema ni kuzidiwa na hali.
Kufikia usiku walimpoteza mtoto wao na sasa kilichosalia ni makovu ya makabiliano dhidi ya polisi na waandamanaji