Kijiji kimoja katika eneo la Kikuyu nchini Kenya kimekumbwa na mshtuko baada ya mwanamke kudaiwa kuwaua watoto wake watatu.
Mwanamke huyo anasemekana kuwalisha sumu watoto wake watatu wenye umri wa miaka 4, mitatu na sita kabla ya kujaribu kujiua.
Hata hivyo hakufanikiwa katika njama yake na kuokolewa na majirani ambao walisema wanashuku kuwa mshukiwa wa mauaji alikumbwa na matatizo ya kiakili kwani alijitenga nao alipokuwa nyumbani kwake.
"Huyo mama amekuwa na kisirani fulani tusemehata akiwa na watoto hapa hakubalii watoto kukanyanga hata nje.
Watoto wanashinda kwa nyumba na yeye mwenyewe, huwa hawatoki unless anaenda dukani," Godfrey Mwanja, ambaye ni jirani aliambia Citizen TV.
Miili ya watoto hao imepelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Thogoto huku mama yao akizuiliwa katika Kituo cha polisi cha Kikuyu uchunguzi wa mauaji hayo ukiendelea.
Kamanda wa polisi wa Kaunti ya Kikuyu Ronald Kirui alithibitisha kisa hicho akisema mama huyo yuko rumande kusaidia katika uchunguzi.
Kirui pia alieleza kuwa uchunguzi wa awali ulitambua kwamba kulikuwepo ugomvi wa kifamilia ambao umekuwa kwa muda mrefu.
"Mama huyo alitaka kujitoa uhai lakini kwa bahati nzuri majirani walikuja kumuokoa na tunaye chini ya ulinzi wetu, atatueleza zaidi kilichojiri lakini kutokana na uchunguzi wa awali tunaamini kuwa hii inawezekana ikawa ni familia, mzozo ambao umeibuka baada ya muda," Kirui alisema.