Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya linamshikilia Zawadi Sastoni Nzunje (30) Mkazi wa Igalako Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya kwa tuhuma za kumuua mtoto wake wa kambo aitwaye Meshaki Fazili Mlawa (12) Mkazi wa Kapyo kwa kumpiga kwa kitu kizito kichwani na kukimbilia kusikojulikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema "Awali Aprili 02, 2023, mtuhumiwa alitoweka nyumbani kwake akiwa na mtoto huyo kwenda naye kusikojulikana ambapo Aprili 04, 2023 ilifunguliwa kesi ya wizi wa mtoto katika kituo cha Polisi Igurusi. Kutokana na tukio hilo, tulianza msako mkali na Aprili 06, 2023 tulimkamata mtuhumiwa."
Amesema "Mtuhumiwa alikamatwa akiwa amejificha au kuomba hifadhi Msikitini na akiwa amevaa mavazi ya kanzu ili aonekane ni muumini mzuri."
Aidha imeelezwa kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hili ni mgogoro kati ya mtuhumiwa na mke wake ambao ulipelekea chuki na hasira dhidi ya mtoto huyo ndipo mtuhumiwa akapanga kumuua mtoto huyo ili kumkomoa aliyekuwa mke wake. Upelelezi unaendelea na mara baada ya kukamilika atafikishwa mahakamani.