Polisi nchini Uganda waliwazuia wabunge 11 wa kike siku ya Alhamisi ambao waliwashutumu kwa kufanya maandamano kinyume cha sheria, huku baadhi ya wabunge hao wakipata majeraha wakati wa kukamatwa kwao.
Wabunge hao walizuiliwa nje kidogo ya majengo ya bunge katika mji mkuu Kampala walipokuwa wakijiandaa kuandamana hadi Wizara ya Mambo ya Ndani ambapo walinuia kukabidhi barua ya maandamano kwa waziri.
Walikuwa wakipinga kile walichosema ni ukatili wa polisi na matumizi ya nguvu kupita kiasi katika matukio mbalimbali yanayoandaliwa na wabunge wanawake katika majimbo yao ya ndani wiki za hivi karibuni.
"Ninalaani vikali namna polisi asubuhi walivyowakamata wabunge 11 wanawake waliokuwa wanafanya maandamano ya amani na wasio na silaha. Wengine wanavuja damu na kwa wengine nguo zilichanika. Ni kana kwamba wanakamata magaidi," naibu spika wa bunge Thomas Tayebwa aliandika katika ukurasa wake wa Twitter.
Video za mzozo huo zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha maafisa wa polisi wakihangaika kuwasukuma wabunge hao ambao wote walikuwa wamevalia mavazi meusi kwenye gari.
Hata hivyo, Wabunge hao waliachiwa bila masharti, kufuatia mazungumzo kati ya uongozi wa polisi na Spika wa Bunge, ambaye aliweleza kuwa wanatakiwa kutoa taarifa ofisini kwake kwanza linapokuja suala la kukamatwa kwa wabunge.