Shule ya msingi Sekaza Memorial iliyopo kata ya Kiringente, Wilaya ya Mpigi nchini Uganda imefungwa kwa muda usiojulikana kufuatia taarifa kuwa kuna mapepo yanawashambulia wanafunzi.
Uongozi wa shule hiyo umesema baadhi ya wanafunzi katika wiki kadhaa zilizopita hawakuweza kuhudhuria masomo wakilalamika kusumbuliwa na magonjwa ya ajabu ambayo wahudumu wa afya wameshindwa kuyagundua.
Kwa mujibu wa tovuti ya Monitor ya nchini humo imeripoti kuwa, taarifa ya kufungwa kwa shule imetangazwa jana Jumatano kufuatia mkutano wa viongozi wa eneo hilo pamoja na Polisi.
"Hatujafundisha masomo tangu wanafunzi warudi kutoka likizo ya Pasaka kwa sababu walikataa kwenda kwenye madarasa yao. Wasimamizi waliona inafaa kuwarejesha nyumbani kwao ili tupate muda wa kutatua tatizo hili,” Julliet Namagembe, ambaye ni Makamu Mkuu wa Shule hiyo.
Namagembe amesema kuna changamoto ambayo kila anayeshikwa na pepo anakosa msaada kwa sababu yeyote atakayejitolea kumsaidia na yeye pia pepo humvaa.
Kulingana na mmoja wa walimu wa muda mrefu wa shule hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema baadhi ya wanafunzi wameonekana kama wana matatizo ya kiakili, ambapo wamekuwa wakipiga kelele na kurukaruka, huku wengine wakiwa dhaifu sana kimwili.
Jana Jumatano, kundi la wazazi waliokuwa na hasira walivamia shule hiyo wakitaka kujua kilichowapata watoto wao. Walijaribu kumfanyia fujo mwalimu mkuu, lakini Polisi waliingilia kati haraka na kuwatuliza.
Afisa wa Polisi wa eneo hilo Ronald Mugarura aliyeongoza kuwatuliza wazazi hao alisema baada ya makubaliano waliamua kushauri wanafunzi wote warudi majumbani mwao kwani suala hilo linatatuliwa.