Siku 678 za msoto wa Sabaya gerezani mpaka kuachiwa

0

 Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya  Aprili 5, 2023 ameachiwa huru baada ya kusota gerezani kwa takribani siku 678, takriban miaka miwili.


Safari ya Sabaya kuanza maisha ya gerezani ilianza rasmi mara baada ya kukamatwa na polisi Kinondoni jijini Dar es Salaam Mei 27, 2021 na kwenda kukabiliwa na mashtaka ya Unyang’anyi wa Kutumia Silaha jijini Arusha.

Ilikuwa ni Juni 4, 2021 ndipo Sabaya na wenzake wawili Sylvester Nyegu na Daniel Mbura walifikiswa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na kesi ikaanza kuunguruma.

Oktoba 15, 2021 Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Arusha, Odira Amworo alisema ameridhika kuwa upande wa mashtaka umethibitisha mashtaka dhidi ya Sabaya na wenzake na kumhukumu kifungo cha miaka 30 jela.

Hukumu hiyo ilikuja mara baada ya Agosti 24, 2021, Sabaya na wenzake kukamilisha kujitetea mahakamani hapo baada ya Jamhuri kukamilisha mashahidi 11 na vielelezo vinane.

Baada ya hukumu hiyo, Mei 6, 2022, Sabaya na wenzake walikata Rufaa katika Mahakama ya Rufaa ya Arusha kupinga hukumu hiyo ya miaka 30 na kufanikiwa kushinda Juni 10, 2022.

Hata hivyo, baada ya Sabaya kushinda, upande wa Jamhuri ulikata Rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha na kesi hiyo bado haijatolewa hukumu yake mpaka sasa.

Wakati Sabaya akiwa ameshinda rufaa yake na kuwekewa kipingamizi na Jamhuri, akawa amesalia na kihunzi kingine Moshi mkoani Kilimanjaro kwani nako alifunguliwa mashtaka mengine.

Juni Mosi, 2022, Sabaya na wenzake wanne walifikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Moshi wakikabiliwa na mashitaka saba ikiwemo uhujumu uchumi. Kesi ikaanza kuunguruma.

Septemba 6, 2022, mahakama hiyo iliwaachia huru washirika wa wanne wa Sabaya, Sylivester Nyegu, John Aweyo, Nathan Msuya na Antero Assey baada ya kukiri kutenda makosa ya uhujumu uchumi ambapo mahakama iliwatia hatiani na kuwaamuru kulipa kila mmoja faini ya Sh50,000 na fidia ya Sh1milioni kwa mwathirika wa tukio hilo ambaye ni Alex Swai.

Hatimaye, leo Aprili 5, 2023, akiwa ametimiza siku 678 za kusota mahabusu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, imemuachia kwa masharti ya kutofanya kosa la jinai kwa kipindi cha mwaka mmoja na kulipa fidia ya Sh 5 milioni aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya baada ya kukiri kosa la kula njama na kuzuia utekelezaji wa haki na kosa la pili kudhania madaraka ambayo si yake.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Salome Mshasha baada ya kumtia hatiani Sabaya aliyekiri kutenda makosa hayo.

Sabaya na wenzake wakiwa eneo la Mboso lililoko Kata ya Masama wilayani Hai bila kufuata sheria walifanya upekuzi nyumbani kwa mfanyabiashara Alex Swai na kujipatia Sh50 milioni kinyume cha sharia.

Kosa la pili Sabaya na wenzake katika maeneo ya mkoa wa Kilimanjaro na Arusha, kwa nia ovu walimkamata Swai kwa madai ya kukwepa kodi ambapo kisheria hawakuwa na mamlaka hayo.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Sabaya anayetetewa na mawakili Moses Mahuna na Hellen Mahuna, alikiri kutenda makosa hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Salome Mshasha na hivyo mahakama ikamtia hatiani kwa makosa hayo.

Katika hukumu hiyo, Hakimu Mshasha alimwamuru Sabaya kulipa fidia ya Sh5 milioni kwa Elibariki Swai ambaye ni ndugu na Alex Swai na pia akamwamuru Sabaya kuhakikisha hafanyi kosa lolote la jinai kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Awali, Sabaya alisomewa mashtaka yake na alikiri kutenda makosa hayo na hakimu alimhukumu kulingana na makubaliano (Plea bargaining) aliyoingia na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) ambaye alimfutia mashtaka ya uhujumu uchumi.

Baada ya kesi hiyo ya awali namba 2/2022 kufutwa na Hakimu Mshasha, mwendesha mashitaka ambaye ni wakili wa Serikali kutoka ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), Veridiana Mlenza alimsomea Sabaya mashtaka mapya mawili.

Awali, katika kesi hiyo namba 2/2022, ilikuwa na jumla ya makosa saba na washtakiwa watano ambapo Sabaya mwenyewe alikuwa na mashtaka matano kabla ya kesi hiyo kufutwa jana na kufunguliwa kesi mpya ya jinai.

Akimsomea mashtaka hayo ambayo ni sehemu ya makubaliano na DPP, wakili Mlenza amesema Januari 19, 2021, Sabaya na washirika wake wanne ambao tayari walishatiwa hatiani mwaka jana, walijipa mamlaka wasiyostahili.

Baada ya kukamilika kwa mchakato huo, saa 9 alasiri Sabaya alitoka chumba cha mahakama akiwa amefuatana na askari polisi na kupanda gari aina ya Toyota Alphard na kuondoka katika eneo la mahakama akiacha karandika la Magereza.

Tunamtakiwa kila la kheri katika maisha yake mapya ya uraia tena.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

JIUNGE NA IDAWA MEDIA SASA
Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Telegram na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka IDAWA TV Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube & Jiunge WhatsApp 

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top