Wananchi wachangishana fedha kukarabati barabara...

0

 Wananchi wa baadhi ya vijiji vilivyopo katika kata ya Matamba wilayani Makete mkoani Njombe wameamua kuchangishana fedha zitumike kufanya ukarabati wa kufukia shimo lililochimbika katikati ya barabara ya Matamba-Chimala


Kuchimbika kwa shimo hilo kulikochangiwa na mvua zinazoendelea kunyesha, kumepelekea magari yanayopita kwenye barabara hiyo yanayosafirisha mazao ya chakula hususan viazi kupita kwa tabu katika eneo hilo

Mkazi wa kijiji hicho Zuberi Mahenge aliyezungumza na Green Fm amesema mbali na shimo hilo lililochimbika barabarani ambalo utaratibu huu wa kulifukia unaendelea kwa wananchi kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo, amesema anafanya kazi ya kuendesha bodaboda lakini hutumia muda na gharama zake kufukia mashimo yaliyopo kwenye barabara hiyo

"Nikipata mteja wa kumpekela Chimala nikimfikisha natumia fedha niliyoipata najaza mafuta kwenye pikipiki nabakisha fedha kidogo ya matumizi, halafu nakwenda kufukia mashimo barabarani, na nimeanza kufanya hivyo muda mrefu kwa sababu nikiwaambia wenzangu wananiambia hawawezi kufanya hivyo kwa sababu hiyo ni kazi ya serikali" amesema Zuberi

Ibrahim Ngogo ni miongoni mwa wachangiaji wa fedha za ukarabati huo ameshukuru kwa wadau kuendelea kuchangia kupitia makundi ya WhatsApp akiwemo Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Makete William Makufwe na kuiomba serikali kuifanyia matengenezo ya kina barabara hiyo badala ya kuijenga kwa kilomita chache chache ili idumu kwa muda mrefu

Sainel Nyambo ni Diwani wa Kata ya Matamba amesema ni kweli wananchi wameamua kujitoa kufanya matengenezo ya eneo hilo huku wakiisubiri serikali iifanyie matengenezo kwa kuwa tayari alishafikisha suala hilo serikalini

Amesema kupitia mitandao ya kijamii kuna watu wamekuwa wakisambaza picha zinazoweza kuzua taharuki na kulifanya jambo hilo kuwa ni kubwa, badala yake amesema ni kweli kunachangamoto lakini sio kubwa kama inavyodhaniwa

Amesema tayari TARURA Makete wanalifahamu tatizo hilo kwa kuwa ameshawafikishia taarifa na kuahidi kuitatua kwani serikali ni sikivu na tangu aingine madarakani amekuwa akifuatilia na barabara hiyo imekuwa ikifanyiwa matengenezo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 


 

 
#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top