Kamati ya chakula ya shule ya msingi Tandala wilayani Makete mkoani Njombe imeeleza kusikitishwa na mwenendo usioridhisha wa baadhi ya wazazi na walezi katika uchangiaji wa chakula cha wanafunzi shuleni hapo.
Akizungumza na Green fm Mwenyekiti wa kamati ya chakula shule ya msingi Tandala Kastory Sanga amesema kwa mujibu wa makubaliano ya mkutano mkuu wa wazazi,mwisho wa kufikisha michango ya chakula kwa kila mzazi ilikuwa ni Machi 15,mwaka huu lakini cha kushangaza mpaka sasa kuna baadhi ya wazazi ambao hawajakamilisha michango hiyo
Amesema kamati imetoa siku 7 kuanzia Jumatano ya Aprili 12, 2023 hadi Jumatano ya Aprili 19 kila mzazi ambaye bado hajawasilisha michango ya chakula kukamilisha haraka na kwa wale ambao watakuwa bado baada ya muda huo majina yao yatafikishwa kwenye serikali ya kijiji kwa hatua zaidi
Kutokana na kujirudia mara kwa mara kwa changamoto ya baadhi ya wazazi kukiuka makubaliano ya kuwasilisha michango ya chakula shuleni hapo Mwenyekiti huyo wa kamati ya chakula ametoa ushauri kwa wazazi na walezi kujenga utamaduni wa kutoa michango ya chakula kipindi cha mavuno badala ya kusubiri mwishoni wakati chakula ndani ya nyumba kimepungua.
Andowise Memba ni miongoni mwa wazazi waliozungumza na kituo hiki ambapo wamesema jukumu la kukusanya chakula kufuatilia kwa makini kwani baadhi ya wazazi wanahitaji kukumbushwa mara kwa mara pasipo kufanya hivyo inaweza kuwa ni vigumu kufikia lengo kwani chakula ni muhimu katika kukuza taaluma ya wanafunzi shuleni.
Yusuph Ilomo ni Mwenyekiti wa kijiji cha Tandala ameeleza hatua ambazo wamekuwa wakizichukua kwa wazazi na walezi ambao wamekuwa wasumbufu kuchangia chakula cha watoto wao shuleni kulingana na makubaliano ya wazazi.