ZANZIBAR.
KATIKA kuhakikisha lengo la ushiriki sawa wa wanawake kwenye
nafasi za uongozi linafikiwa, wanawake wenye nia ya kugombea na kushika nafasi
hizo wametakiwa kutumia muda wao kukaa karibu na jamii zao ili kubaini
changamoto zinazowakabili wananchi na kusaidia kuzitaftia ufumbuzi badala ya
kusubiri kipindi cha uchaguzi.
Imeelezwa kuwa suala la ushiriki kugombea nafasi za uongozi
ni mchakato endelevu ambao unahitaji maadalizi ya muda mrefu bila kusubiri
kufanya maandalizi hayo kipindi cha uchaguzi kinapokaribia jambo ambalo
linapelekea jamii kukosa inami nao.
Hayo yameelezwa na wadau wa usawa wa kijinsia wakati wa
mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo wanawake 35 wenye dhamira ya kugombea kutoka
vyama mbalimbali vya siasa kisiwani Pemba yaliyoandaliwa na Chama Cha Wandhishi
wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa kushirikiana na Ubalozi
wa Norway kutambua misingi, taratibu, wajibu na hatua muhimu za kufuatwa kabla
na wakati wa kugombea ili kuwa kiongozi bora katika jamii.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo Dkt. Salum Suleiman Ali, kutoka
Chuo kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) alisema wanawake wanayo nguvu ya ushawishi
na iwapo watajua namna ya kuitumia kwa kujenga hoja na kuwa karibu na jamii
itawasaidia kufikia malengo na kushika nafasi za uongozi katika ngazi
mbalimbali bila vikwazo.
“Wanawake lazima kwanza tuwe na uwezo wa kujitayarisha kiuongozi ikiwemo kuyaacha baadhi ya mambo ambayo yanaweza kutumika kukubomoa. Kisha utambue changamoto zilizopo katika jamii na kubaini fursa zilizopo za kuweza kutatua changamoto hizo,” alieleza Dkt. Salum.
Aidha alisema ili kufikia lengo hilo kila mwanamke anatakiwa
kuwa jeshi la kumlinda na kumuongoza mwenzake kwenye masuala ya uongozi ili
kujenga heshima ya wanawake wote kwenye uongozi bila kuharibu heshima ya
wanawake wengine.
“Uongozi kwenye jimbo huendi kumtawala mtu. Kubwa ni kwenda
kusikiliza matatizo na changamoto za watu na kuisaidia jamii kuondokana na
matatizo hayo kazi ambayo inaweza kufanywa muda wowote na kila mmoja awe ni
mwanamke au mwanaume hivyo ili uweze kufanikisha hilo lazima kwanza uwe karibu
na watu wako mapema ili kuzijua vizuri shida zao kwa undani,” alieleza Dkt.
Salum Suleiman Ali.
Aidha alifahamisha, “mafunzo haya yamekuja mapema ambapo bado
miaka miwili kuelekea uchaguzi mkuu kwasababu kuna mambo muhimu unatakiwa
kuyaanza mapema na sio kusubiri uchaguzi umefika ndipo uanze mchakato kwasababu
kwenye siasa sio ujanja bali ni mikakati bora inayolenga kutetea wananchi
unaowaongoza.”
Mapema mratibu wa TAMWA ZNZ ofisi ya Pemba Fat-hiya Mussa
Said aliwataka wanawake kushikamana bila kujali tofauti za vyama vya siasa
lengo likiwa ni kufanikisha kupata idadi kubwa ya wanawake wanaoingia katika
nafasi za uongozi.
Alieleza, “kila mmoja wetu humu tunataka angalau awafikie
wanawake wengine 20 kwenye vyama vyetu na jamii zetu kutoa elimu ili tupate
uwakilishi wa wanawake wengi walio bora na wenye uthubutu wa kusimama na
kuongoza katika nafasi mbalimbali kwa kufuata misingi na maadili yanayotakiwa
kwa kiongozi bora.”
Kwa upande wake mkurugenzi wa Jumuiya ya Utetezi wa Jinsia na
Mazingira Pemba (PEGAO) akizungumzia kuhusu mafunzo hayo yaliyoandaliwa kupitia
mradi wa Wanawake na uongozi alisema yanalenga kuwaandaa wanawake weye nia ya
kugombea nafasi hizo kuwa na uwezo wa kusimama kutatua changamoto zinazoikabili
jamii kabla ya kugombea katika chaguzi mbalimbali.
“Mafunzo haya yameletwa mapema ili tuanze kutumia ujuzi
huu tuliofundishwa kufanya kwa vitendo kwenye jamii kwa kukaa karibu nao
kuzijua changamoto zao ili waamini na kuwaunga mkono katika jambo mnalofanya
kuliko kukaa na kusubiri kipindi cha uchaguzi ndipo unaenda kwenye jamii kutaka
wakuchague kuwa kiongozi wao,” alieleza mkurugenzi huyo.
Zainab Mussa Bakar mmoja wa washiriki kutoka Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Pemba aliwataka wanawake wenye nia ya
kugombea nafasi za uongozi kuwekeza nguvu katika kujijengea uwezo binafsi
ikiwemo kujiendeleza kielimu ili kuepukana na changamoto za udhalilishaji wanazokumbana
nazo kipindi cha uchaguzi.
Alisema, “wanamke tunatakiwa tujiamini na tujitahidi tuwe na
uwezo binafsi hasa kujiendeleza kielimu, tusitegemee mtu katika nafasi za
uongozi na badala yake tutegemee zaidi nguvu na uwezo wetu kwani kumtegemea mtu
atakapoona unafanikiwa kumzidi atatafufa njia ya kukushusha.”
Mafunzo haya maalum ya kuwajengea uwezo wanawake wenye
dhamira ya kugombea nafasi za uongozi yanakuja baada ya kufanyika kwa mikutano
ya uhamasishaji kwenye Shehia iliyofanywa na Wahamasihaji Jamii kuhusu umuhimu
wa wanawake kudai na kushiriki kwenye nafasi za uongozi na wanawake hao
kuhamasika kuwa tayari kugombea nafasi hizo.