Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Njombe Wilferdy Willa ameitaka Jamii Mkoani humo hususani Wanaume kutambua kuwa fedha inayotafutwa na Mwanamke aliye kwenye ndoa ni ya kwake binafsi lakini fedha inayotafutwa na Mwanaume ni ya Familia jambo ambalo litasaidia kutatua migogoro ya ndoa.
Willa amesema hayo katika semina kwa Viongozi iliyoratibiwa na Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Njombe ambapo amesema ni vema Wanaume wakatambua majukumu yao katika Familia kama inavyoeleza sheria ya ndoa kwakuwa itasaidia kupunguza migogoro kwenye ndoa.
Willa amesema Wanaume wengi kwenye ndoa hudhani pesa inayotafutwa na Mwanamke ndani ya ndoa ni ya Familia (wote) jambo ambalo sio sahihi kwa mujibu wa sheria ya ndoa badala yake Mwanamke ana wajibu wa kuwajibika kupitia fedha yake endapo tu Baba hayupo, amefariki au hawezi kutekeleza majukumu kwa wakati huo.
"Mwanaume au Mwanamke ukijua majukumu yako kwenye Familia hakutakuwa na kelele, ukisoma sheria ya ndoa inasema Baba atawajibika kuhakikisha Familia yake inakuwa na ustawi na Mwanamke atafanya majukumu ya Baba kama Baba hayupo au hana uwezo wa kutekeleza majukumu kwa wakati huo, kwahiyo fedha inayotafutwa na Mwananke ni ya kwake na inayotafutwa na Mwanaume ni ya Familia"