Zikiwa zimepita siku 53 tangu aliyekuwa msichana wa kazi za ndani Annet Kassim (20) kudaiwa kuuwawa na bosi wake, mfanyabiashara Diana Sabhai (44), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, akikabiliwa na shtaka la kumuua msaidizi wake.
Februari 9 mwaka huu mwanamke mfanyabiashara huyo, mkazi wa Tabata Kimanga, alidaiwa kumuua msichana wake wa kazi na kisha kusingizia kuwa amejinyonga.
Hata hivyo Jumanne Aprili 5, 2023 mfanyabiashara huyo alifikishwa Mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi, Aneth Nyenyema na kusomewa shtaka hilo na Wakili wa Serikali wa Serikali Agatha Lumato.
Wakili Agatha, alidai mshitakiwa alitenda kosa hilo Februari 9, mwaka huu maeneo ya Tabata Kimanga, Wilaya ya Ilala, ambapo alimuua Aneth Kassim.
Baada ya kusomewa shtaka hilo mshitakiwa hakurusiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya mauaji kwa mujibu wa sheria.
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika, hivyo kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Aneth aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 13, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa na mshtakiwa alirudishwa rumande kutokana na kesi za mauaji kutokuwa na dhamana.