Mkazi wa kata ya Nyamatare Manispaa ya Musoma mkoani Mara, Katembo Mnubi au Wajanga mwenye umri wa miaka 81 amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Musoma akikabiliwa na tuhuma za kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 11, mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi Nyamatare.
Akisoma kesi hiyo mwendesha mashitaka wa serikali Beatrice Mgumba, mbele ya Hakimu wa wilaya ya Musoma Aristeda Tarimo amesema kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Machi 2, 2023 majira ya saa nne za asubuhi kipindi mtoto huyo akiwa katika mapumziko ya vipindi vya darasani.
Tarimo ameiambia mahakama ya Wilaya kuwa mtuhumiwa huyo amekuwa akimtendea unyama mtoto huyo zaidi ya mara moja ambapo siku ya kwanza mtuhumiwa alimwita mtoto huyo akiwa mapumziko ya vipindi vya darasani na kumtaka aende ndani kwakwe akachukue fedha na akamnunulie sigara.
Amesema baada ya mtoto huyo kuingia ndani ndipo mtuhumiwa alipofunga mlango na kukamata kisu ambacho kilikua maeneo ya kitandani na kumuonya kuwa endapo angepiga kelele angelimchoma kisu na baada ya hapo alimvua nguo na yeye pia kuvua nguo na kuanza kumfanyia unyama huo na mwisho kumpa Sh 100.