Bibi wa miaka 62 afia kisimani akijaribu kuchota maji

0

 Anna Keto (62), mkazi wa mtaa wa Mikocheni C Madale amekutwa amefariki, baada ya kudondokea kwenye kisima cha maji kilicho nyuma ya nyumba yake.


Tukio hilo limetokea Aprili 26 mwaka huu, mchana wakati mume wake akiwa ameenda shambani eneo la Kilimahewa.

Akizungumza  Jeni Kipondamalia, ambaye ni jirani alisema, saa saba mchana mumewe aliporudi alienda jikoni na kukuta chakula kimepikwa huku mifugo ikiwa imelishwa lakini mkewe huyo hayupo.

Alisema pembeni ya kisima kilichopo nyuma ya nyumba wanayoishi, alikuta madumu ya maji yakiwa yameegeshwa pembeni, lakini hakutilia shaka akaanza kumtafuta mkewe ili wale lakini hakumuona.

Alisema kutokana na jua kuwa kali, wakati anarudi akaona achukue madumu yaliyokuwa pembeni ya kisima, wakati anachungulia akamuona mkewe ndani ya kisima, ndipo alipoanza kupiga mayowe.

Kipondamalia alisema alisikia yowe lililokuwa likipigwa na mume wa marehemu akiomba msaada.

"Nilifikiri yule bibi kaanguka kutokana na matatizo yake, nilipofika akaniambia angalia ndani ya kisima, nilipochungulia nikamuona yule bibi anaelea nikajua si mzima, nikawapigia majirani, walipokuja tukasema tutafute ngazi lakini hii ni kesi ya polisi," alisema.

Alifafanua kuwa baadhi ya majirani walimjulisha Mwenyekiti wa kijiji na kutoa taarifa polisi, hata hivyo walifika kwa wakati na kuutoa mwili huo.

Naye Isaya Mng'anga, jirani wa familia hiyo, alisema, "Nilifika hapa (jana) juzi baada ya kusikia kelele, ndipo nikakuta huyu bibi yuko ndani ya kisima, juhudi za kumtoa zilianza kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, na baadaye mwili wake ulipelekwa Hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya uchunguzi," alisema Mng'anga.

Akizungumza nasi, mume wa marehemu, Daudi Keto alisema mke wake alikuwa mgonjwa tangu mwaka 2015.

Alisema siku ya tukio aliondoka asubuhi na kumwacha mkewe akiendelea na majukumu yake kama kawaida, na aliporudi mchana hakumuona, alikuta mifugo imelishwa na madumu ya maji yakiwa pembeni ya kisima.

"Nilimtafuta ndani sikumuona nikajua yuko kwenye biashara zake za ndimu, nilizunguka nyuma ya nyumba lakini sikumuona, baadaye wakati nachukua madumu kuangalia kwenye kisima nikamuona anaelea," alisema.

Marehemu ameacha watoto watatu, akiwamo wa kike mmoja. Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Mtatiro Kitinkwi alisema anaendelea kufuatilia taarifa ya tukio hilo na atalitolea taarifa atakapopata usahihi wake.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 


 

 
#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top