Baada ya kushindwa katika shauri lake Feisal Salum Abdallah (Fei Toto) alilolipeleka TFF ili kuomba kuvunja mkataba wake na Yanga,Mchezaji huo kupitia ukurasa wake wa Instagram ameanza kampeni ya kuomba michango ili kufanikisha ndoto yake ya kwenda CAS kupata haki yake.
Katika ujumbe alioshirikisha katika Mitandao Feisal Salum Abdallah (Fei Toto) amesema kuwa TFF imeshindwa kumsaidia na huu ndio ujumbe wake kwa wadau wanaoweza kumchangia.
“Ndugu zangu Watanzania na familia yote ya soka kwa
Bara na visiwani. Mimi kijana wenu ambaye kwa miaka yote nimekua na nidhamu nje na ndani ya uwanja na kwa dhati nimeitumikia klabu ya Yanga na Timu ya Taifa ya Tanzania na Zanzibar Heros.
Utiifu wangu umekua shubiri ya maisha yangu ya soka, nimevumilia nimeshindwa, sitamani tena mama vangu kutukanwa. TFF imeshindwa kunisaidia kupata haki yangu ya Kuvunja mkataba na Yanga hivyo nimeamua Kwenda Mahakama ya michezo CAS.
Nahitaji Mchango wa kila Mtanzania mpenda haki na maendeleo ya wachezaji wa Kitanzania ambao wamekua kimya na woga juu ya maslahi, Heshima na Haki zao. Naomba unichangie kadiri utakavyoweza ili niweze kupata pesa ya Kulipia gharama za kufungua Jalada la kesi yangu CAS ili kupata Haki yangu ya
Kuondoka Yanga kwa kuvunja mkataba.
Tafadhali naomba unichangie ili nipate haki yangu itakayoniwezesha kutumikia kipaji changu na Timu za Taifa (Tanzania na Zanzibar) katika namna tofauti kwa manufaa yangu na Taifa,” ameandika Feisal Salum Abdallah (Fei Toto)