Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Ileje mkoani Songwe limeiomba Serikali kupitia upya Sheria inayohusu michezo ya kubashiri kutokana na kusababisha kuvunjika kwa ndoa na kuibuka vitendo vya uharifu kwa vijana wilayani hapo.
Diwani viti maalum, Subira Kyomo alitoa ombi hilo Aprili 29,2023 katika kikao cha baraza la madiwani cha robo ya tatu cha kupitia na kujadili taarifa ya mwaka wa fedha 2022/2023 kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo .
Kyomo, amesema michezo ya kubahatisha imekuwa na athari kubwa kwa jamii ikiwepo mmonyoko wa maadili kwa vijana na ongezeko la vitendo vya uharifu na ndoa kuvunjia na kukosa suluhisho.
“Tunapokea malalamiko mengi yanayohusu migogoro ya ndoa hasa kwenye kundi la vijana, huku sababu kubwa ikionekana ni michezo ya kubahatisha,” amesema.
Diwani wa Kata ya Itumba Mohamed Mwala alimuunga mkono Kyomo na kusema idadi kubwa ya vijana wanashindwa kujikita katika shughuli za uzalishaji mali hususan kwenye kilimo na badala yake kugeukia mashine za michezo ya kubashiri.
“Ingawa kuna mapato tunaingiza lakini michezo hiyo inapoteza nguvu kazi kwa Taifa kwani tunaona vijana na wanandoa wakiwa na migogoro, kutokana na hali hiyo tunaiomba Serikali ilichukulie jambo hili kwa ukubwa,”amesema Mwala .
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Songwe, Ubatizo Songa alisema watawasilisha ombi hilo serikalini ili kuweza kutafuta mwarobaini wa kupitia upya sheria ya michezo ya kubahatisha ili kuokoa kizazi cha sasa na kijacho .
Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farida Magomi aliwataka madiwani kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na madhara yatokanayo na michezo ya kubahatisha badala yake wageukie shughuli za kiuchumi.