Aliyekuwa Mwanachama wa chama cha Wananchi CUF na aliyewahi kuwa mbunge kupitia Chama hicho Mayeye amekihama chama hicho leo na kujiunga na ACT-Wazalendo.
Katika Tamko alilolitoa kwa waandishi wa Habari Mayeye amesema "Mimi Kiza Mayeye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake CUF (JUKE) ambaye nilikuwa pia Mbunge wa Viti Maalum, nimejiondoa kwenye Chama cha CUF na kujiunga na ACT Wazalendo.
Nimekwishajisajili kwenye mfumo wa kuandikisha wanachama wa ACT Kiganjani, nimelipia aina ya kadi ya Maalim Seif na ada ya uanachama kwa miezi sitini (miaka mitano). Hivyo mimi ni mwanachama kamili wa ACT Wazalendo
Nimekitumikia Chama cha CUF kwa nafasi mbalimbali tangu mwaka 2011 nilipojiunga nacho. Nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipokishukuru Chama cha CUF kwa kunilea kiuongozi na kunipa fursa mbalimbali kukitumikia.
Leo, nimelazimika kuchukua maamuzi haya magumu kwa sababu ambazo haziwezi kuzuilika.
Mosi, mimi ni mwanasiasa wa vitendo. Naamini siasa halisi ipo chini (field), kwa wananchi. Mwaka 2020 niligombea Ubunge katika Jimbo la Kigoma Kaskazini na kwa matokeo halisi nilishinda. Lakini, kilichotokea mwaka 2020 sote tunakifahamu; walioshinda walishindwishwa na walioshindwa walishindishwa!
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilipotangaza kuwa nimekuwa mshindi wa pili kwa kupata kura 16252 kila mmoja alishangaa! Bila shaka hata CCM wenyewe walishangaa, kwa sababu walijua nilishinda!
Ninajiunga ACT Wazalendo ili kuendeleza mapambano. Nimefanya uchambuzi wa kina na kujiridhisha kuwa ACT Wazalendo ndio jahazi sahihi la kuendeleza harakati zangu kwa ajili ya kuwakomboa wanachi wa Kigoma Kaskazini, Mkoa mzima wa Kigoma na Tanzania kwa ujumla.
Nimevutiwa sana na sera za ACT Wazalendo za kujenga Tanzania ya wote kwa maslahi ya wote. Nimeshawishika pia na jitihada za Chama kuimarisha mtandao wake nchi nzima. Nimevutiwa pia na jitihada za Chama kukuza vipaji vya vijana na wanawake.
Kabla sijafanya uamuzi huu nimezungumza na vyama vingi ili kufanya utafiti kabla ya kujiunga na Chama husika. Mwishowe nikafanya hitimisho kuwa ACT Wazalendo ndio jukwaa sahihi. Wale ambao walitarajia nitajiunga nao, waniwie radhi, vigezo vya kisayansi vimenipeleka ACT Wazalendo!
Nimekuja kuongeza nguvu kwenye ujenzi wa Chama katika kujihakikishia ushindi kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.
Ninatarajia kwenda Jimboni Kigoma Kaskazini hivi karibuni. Huko nitaeleza kwa kina zaidi kwa nini Chama hiki kinapaswa kuwa tumaini lao kutokana na utafiti na uchambuzi wa kina nilioufanya.