Watu 12 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha, wakidaiwa kufanya uharibifu katika ofisi ya Serikali ya Kijiji ikiwemo kuchana bendera ya Taifa na kuondoka nayo, huku mmoja akipoteza maisha baada ya ghasia kuzuka baina ya wavuvi na askari wa uhifadhi.
Watu hao wanadaiwa pia kuvamia ofisi na makazi ya askari wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), zilizopo eneo la Mto wa Mbu, Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha na kufanya uharibifu mali za Shirika hilo yakiwemo magari.
Uharibufu mwingine umetajwa kuwa ni upangaji wa mawe barabarani na hivyo kuzuia watumiaji wengine wa barabara wasiendelee na shughuli zao, kwa madai kuwa, wavuvi wenzao wamezamishwa majini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Jumanne Mei 23,2023 na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, imesema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa madai ya wananchi juu ya wavuvi wanaodaiwa kuzamishwa majini na kwamba ukibaini ukweli, wahusika watafikishwa mahakamani.
Taarifa hiyo imesema Mei 22, 2023 saa 5:40 asubuhi katika Kitongoji cha Magomeni, Kijiji cha Jangwani eneo la Mto wa Mbu, Askari wa hifadhi ya Manyara wakiwa katika doria ya kawaida eneo la Ziwa Manyara walikamata wavuvi watatu waliokuwa wakivua samaki katika maeneo yaliyozuiliwa na uhifadhi.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa walijitokeza wavuvi wengine na kuzusha vurugu iliyosababisha askari hao kushindwa kuwachukua watuhumiwa hao na kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi.
"Umati wa watu hao walikwenda hadi kwenye ofisi ya kijiji cha Jangwani na kufanya uharibifu mkubwa katika ofisi hiyo ya serikali kwa kuvunja madirisha pamoja na kuchana bendera ya taifa na kuondoka nayo kwa madai kuwa wavuvi wenzao wamezamishwa maji wakati wanakamatwa na askari wa uhifadhi," imesomeka sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza;
"Baada ya uharibifu huo kundi hilo liliamua kuelekea ofisi na makazi ya askari wa Tanapa yaliyopo Mto wa Mbu, watu hao wakiwa wanaelekea kuvamia ofisi na makazi hayo njiani walifanya uharibifu mkubwa wa magari kwa kutumia rungu na mawe pamoja na kupanga mawe barabarani kuzuia watumiaji wengine wa barabara wasiendelee na shughuli zao."
Taarifa hiyo imeeleza kuwa licha ya juhudi za kuwazuia wananchi hao kuingia katika ofisi na makazi hayo ya askari wa Tanapa, watu hao waliendelea kupambana na askari wa uhifadhi, hivyo kuhitajika jeshi la polisi kuongeza nguvu ili madhara zaidi yasitokee.
Taarifa ya Jeshi hilo imesema kuwa kutokana na ghasia hizo, mtu mmoja alipoteza maisha na watu saba wamelazwa huku wakiendelea na matibabu.
Kwa upand mwingine, jeshi hilo limeonya juu ya tabia ya badhi ya watu kupambana na vyombo vya dola ambavyo kimsingi wamepewa dhamana ya kulinda maisha ya watu na mali zao na kwamba endapo kuna changamoto yoyote, zipo taratibu za kufuata na siyo kufanya vurugu au kujichukulia sheria mkononi.
Jana Mkuu wa Wilaya ya Monduli Joshua Nassari alithibitisha tukio hilo huku Diwani wa Kata ya Mto wa Mbu, Hussein Munga, akieleza kuwa kulikuwa na mgogoro baina ya wavuvi wa Kijiji cha Jangwani na hifadhi hiyo ambapo uliingiliwa kati na Mkuu huyo wa Wilaya kwa ajili ya utatuzi.
"Baada ya kufanya vikao viwili iligundulika kuwa wavuvi walichokuwa wanahitaji pale ni mpaka, bahati nzuri Mkuu wa wilaya ameisha chukua hatua kwa kuagiza wapimaji kutoka halmashauri kuweka alama za mipaka kwa maana ya maboya, alituma timu kutoka halmashauri ikaja eneo lile," amesema Diwani huyo.
Alidai kuwa wiki iliyopita mpaka uliwekwa katika eneo hilo ila wavuvi hao hawakuridhika na kudai mpaka umesogea Zaidi kwao.
Akizungumzia tukio hilo kwa njia ya simu, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela, alieleza kuwa yuko nje ya mkoa na alikuwa njiani kuelekea eneo hilo la tukio.