Pikipiki ambayo jina la mmiliki wala namba zake hajafahamika mara moja imelipuka na kuteketea kwa moto katika tukio lililotokea eneo la kituo cha mabasi madogo ya Posta jijini Mwanza.
Akizungumza muda mfupi baada ya pikipiki hiyo
ambayo hata dereva wake hakufahamika, Faustine Magiri, mmoja wa mashuhuda
amesema kabla ya kulipuka moto, pikipiki hiyo iliyokuwa ikitokea njia ya
Nyegezi kupitia barabara kuu ya Kenyatta ilikuwa ikivuja mafuta ambayo yaliacha
michirizi barabarani.
“Pikipiki ile iliwaka moto na kuanza kuteketea
likiwa bado linatembea ndipo dereva akalisimamisha na kuruka kuepuka kuungua,”
amesema Faustini Magiri, anayemiliki duka la vifaa vya ujenzi karibu na eneo la
tukio
Amesema pikipiki hiyo ilishika moto wakati dereva
wake alipokuwa akielekea kwenye duka lake ndipo alipompigia kelele kumgutusha
ashuke asiungue.
"Tulivyofuatilia, tuligundua pikipiki ile
ilikuwa ikimwaga mafuta na kwa bahati mbaya dereva hakushtuka hadi ilipolipuka
na kuteketea,” amesema Magiri
Amesema kukosa elimu na uelewa mpana wa namna ya
kukabiliana na majanga ya moto ndio kumesababisha pikipiki hiyo kuteketea kwa
sababu licha ya watu kujitokeza mapema, hakuna aliyeweza kusaidia kuzima moto
huo.
“Mmoja wa wananchi alikuja nan doo ya maji na
kumwagia pikipiki iliyokuwa ikiteketea; badala ya kuzimika, moto ukaongezeka
mara dufu. Wananchi wangekuwa na elimu ya kutosha ya kukabiliana na majanga ya
moto wangetumia mchanga au blanketi kufunika pikipiki ile kupunguza hewa ya
Oksijeni ili moto uzimike,’’ amesema Hellene Zablon, mjasiriamali anayeuza
mihogo ya kukaanga eneo la Posta
Juma Masanja, mmoja wa wafanyabiashara ndogo ndogo
maarufu kama Machinga amewashauri wamiliki na madereva wa vyombo vya moto
kujenga utamaduni wa kukagua vyombo vya kujiridhisha na ubora na usalama kabla
na baada ya safari.