Serikali yaanza uchunguzi kiwanda kilichojeruhi sita Arusha

0

Serikali imeanza uchunguzi kubaini uhalali wa kiwanda cha kutengeneza mikate cha ‘Kiranyi Bakery’ kilichopo eneo la Kiranyi wilayani Arumeru mkoani Arusha ambapo jana kilikubwa na mlipuko uliotokana na gesi na kujeruhi watu sita.


Mlipuko huo uliotokea jana Mei 9, 2023 umeharibu kiwanda chote baada ya mtungi uliokuwa ukiongezewa gesi kulipuka huku mingine mitatu ikiokolewa na maofisa za Jeshi la Zimamoto.

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Emmanuela Kaganda akizungumza na mwananchi leo Mei 10,2023 amesema uchunguzi umeanza kubaini uhalali wa kiwanda hicho kilichopo katikati ya makazi ya watu.

"Tunachunguza kama walikuwa na vibali vyote maana yale mazingira kilipo kiwanda hatudhani kama ni sawa japo tumekuwa tukihimiza uanzishwaji viwanda vidogo," amesema.

Kaganda amesema watu sita wamebainika kujeruhiwa na moto uliowaka katika kiwanda hicho na kuteketeza mashine zote.

"Hadi leo watu sita wamebainika kujeruhiwa akiwepo mmiliki wa kiwanda hicho, dereva wa gari la kampuni ya kusambaza gesi na wafanyakazi " amesema

Amesema majeruhi hao wamelazwa Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru iliyopo jijini Arusha.

Mwenyekiti wa mtaa wa Kiranyi, Julius Lalaitu amesema mlipuko mkubwa umeteketeza kiwanda hicho kilipo mtaani kwake.

"Tulifika mapema eneo la tukio watu wameungua na walikimbizwa hospitali hata hivyo kuhusu uhalali na leseni Mimi siwezi kujua" amesema.

Mmoja wa majirani wa kiwanda hicho, John Layani amesema wakati mlipuko unatokea kulikuwa na wafanyakazi ndani wanaofika 12.

"Nawajua vijana wanaofanya kazi hapa kiwandani, moto ulilipuka ghafla na walianza kukimbia na kama sio jitihada za kikosi cha Zimamoto ungeleta maafa zaidi" amesema
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top