Serikali Mkoani Mbeya Katika kuendeleza mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe Juma Homera ameagiza wamiliki wa kumbi zote za starehe, Hoteli na Bar Mkoani Mbeya, kuhakikisha wanaweka kondom katika maeneo yaliyotengwa Ili kutoa nafasi kwa wananchi kujikinga dhidi ya maambukizi hayo.
Homera ametoa magizo hayo katika kikao cha kujadili utekelezaji wa afua mbalimbali za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Ukimwi Mkoani Mbeya, ikijumuisha Wadau kutoka maeneo mbalimbali hapa Nchini, ambapo amesema kwa mujibu wa utafiti Mkoa wa Mbeya unashika nafasi ya tatu katika maambukizi ya VVU ikitanguliwa na Mikoa ya Njombe na Iringa, huku waathirika wakubwa wakiwa ni vijana wa miaka 15-24.
Amesema kwa Mkoa wa Mbeya watu 109,332 kati ya watu 142,493 wanaokadiliwa kuwa wanaishi na maambukizi ya VVU wamepima afya huku wakifanikiwa kutoa dawa za kufubaza makali ya virusi hivyo kwa watu 108,197 kati ya watu 109,332 waliogunduliwa kuwa na virusi vya Ukimwi.