Serikali imewafutia leseni baadhi ya wahudumu wa afya waliohusika na tukio la kusababisha kifo cha mama na mtoto katika wodi ya wazazi hospitali ya rufaa Mnazimmoja Mei 15 mwaka huu.
Akitoa taarifa ya ripoti ya uchunguzi iliyofanywa na Baraza la Madaktari Naibu Waziri wa Wizara Hassan Khamis Hafidh, amesema uchunguzi ubaini kuwa wahudumu wa afya watatu wamehusika na kifo cha mama huyo kutokana na uzembe walioufanya kwa mujibu wa sheria namba 12 ya mwaka 1999 ya Baraza la Madaktari.
Akiwataja wahudumu hao kuwa ni pamoja na Riziki Suleiman Yussuf ambae alijitambulisha kuwa daktari (Medical Doctor), Dkt. Salamuu Rashid Ali na Dkt. Nihifadh Issa Kassim ambae ni Daktari Bingwa.
Sambamba na hayo alisema baraza pia limemuona hana hatia Dk. Massoud Omar Hamad kwani alipangiwa kazi chumba cha upasuaji kwa siku hiyo na alitekeleza wajibu wake kama ilivyopaswa.
Amesema watendaji hao kwa mujibu wa sheria ya baraza wanatakiwa kuomba upya na kufuata taratibu zote lakini hivi sasa hawatakiwi kufanya kazi popote duniani na mishahara yao imeshafungwa mara moja kuanzia jana.