JESHI la Polisi, mkoani Mwanza linamshikilia Herman Magigita (60) mkazi wa Kijiji cha Chema, Tarafa ya Kahunda, Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza kwa tuhuma za kutoa mahubiri yenye kupotosha jamii.
Mtuhumiwa huyo ambaye ni mchungaji wa kanisa liitwalo NENO, alikamtwa baada ya kutoa mahubiri ya kupotosha waumini wake wasiende hospitali kupata matibabu pindi wanapougu, badala yake wawapeleke katika kanisa hilo kwa ajili ya maombezi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroard Mutafungwa, ameeleza kuwa mtuhumiwa huyo alikamtwa baada ya jeshi hilo kupata taarifa za uwepo wa mchungaji huyo anayetoa mahubiri ya kupotosha na kufanya shughuli za kanisa bila kuwa na kibali cha usajili.
"Tulipata taarifa kuwa kuna mtu anatoa mahubiri ya kupotosha jamii, ambapo askari polisi walifika katika kanisa hilo na kufanikiwa kumkamata," alisema Kamanda Mutafungwa.