Familia ya James Sije mkazi wa jijini Mwanza, imewasilisha maombi madogo ya jinai katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), na wenzake sita.
Wajibu maombi wengine katika shauri hilo ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza, mkuu wa upelelezi Mkoa wa Mwanza, mkuu wa polisi Wilaya ya Nyamagana, mkuu wa upelelezi wa Wilaya ya Nyamagana na mkurugenzi wa mashtaka.
Katika shauri hilo la maombi madogo ya jinai namba 28/2023, mleta maombi (James Sije) chini ya kifungu cha 390 (1) (a) na (b) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai anaiomba Mahakama itoe amri kwa wajibu maombi kumfikisha mahakamani iwapo ana tuhuma zinazomkabili.
Mleta maombi ameiomba Mahakama kutoa amri kwa wajibu maombi wanaodaiwa wanamshikilia; wamuachie huru iwapo hana tuhuma zinazomkabili, huku akinakili Ibara ya 15 (1) na (2) ya Katiba ya Tanzania inayosisitiza kuwa kila mtu anastahili kuishi kama mtu huru.
Shauri hilo limetajwa leo Jumatano Septemba 20, 2023 mbele ya Jaji Lilian Itemba. Upande wa mjibu maombi (Jamhuri) uliwakilishwa na wakili Evance Kaisi kwa niaba ya mwendesha mashtaka wa Serikali, George Ngemela ambaye hakufika mahakamani kutokana na kufiwa na baba yake mzazi Alhamisi 14, 2023.
Kutokana na mwendesha mashtaka wa Serikali anayesimamia shauri hilo kutokuwapo mahakamani, Jaji Lilian ameahirisha shauri hilo hadi Septemba 25, mwaka huu litakaposikilizwa, huku akiiagiza Jamhuri kuwasilisha kiapo cha pingamizi la maombi hayo ndani ya siku tatu .
Akizungumza baada ya shauri hilo kuahirishwa, wakili Peter Madeleka amedai Agosti 17, 2021 kati ya saa 2.30 hadi tatu usiku, Sije akiwa katika baa iliyoko eneo la National, Kata ya Nyakato jijini Mwanza alifuatwa na askari watatu waliomchukua na kutokomea naye kusikojulikana.